MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko amesema serikali ipo tayari kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) katika ujenzi wa Ndaki ya Tiba Kampasi ya Mloganzila, kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Akizungumza leo Novemba 15, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo, DC Bomboko amesema mradi huo utagharimu Sh bilioni 50.
Amesema loti ya kwanza itagharimu Sh bilioni 23 na ya pili Sh bilioni 26. “Bila ya dhamira ya kweli na dhati ndugu zangu fedha hizi zisingekuja kwenye sekta ya afya,” amesema DC Bomboko.
Amesema hatua hiyo ni dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha analinda nguvu kazi ya taifa ya kutengeneza wataalamu wa sayansi ya tiba.
Akizungumza katika halfa hiyo, Mratibu wa Mradi wa HEET Muhas, Profesa Erasto Mbugi amesema licha ya mafaniko waliyonayo ila ufinyu wa miundombinu umekifanya chuo hicho kushindwa kukuwa kwa kasi ndio maana kumekuwa na ongezeko la programu limekuwa dogo kwa kipindi kirefu.
Amesema katika kuendelea kampasi mbili za chuo hicho Kigoma na Mloganzila, Muhas imetengewa Sh bilioni 120 ili kutekeleza miradi hiyo.
Prof Mbugi amesema utekelezaji wa mradi huo umejikita zaidi katika kuboresha miundombinu, kuendeleza wahadhiri katika mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi, kuboresha mitaala ya kufundisha ili kuendena na soko la ajira na mifumo ya Tehama.
Akitoa taarifa fupi za mradi huo, Prof Mbugi amesema mradi huo ulianza rasmi utaiji saini Juni 2021, na unatarajiwa kukamilika Julai 2026.” Mradi huu unahusisha maeneo saba ya kipaumbele, eneo la kwanza ni ukarabati wa miundombinu, kuboresha mbinu za kufundishia kwa walimu, kuboresha tafiti na ubunifu, kujenga na kuboresha uhusiano na sekta binfasi katika mafunzo, kuboresha mifumo ya Tehama,”
Kuainisha na kuendeleza njia mbalimbali za kuzalisha kipato cha ndani, eneo la mwisho sio kwa umuhimu, kujenga uwezo wa wanataalumana viongozi wa taasisi katika kuyasimamia yote niliyoyasema,” amesema Prof Mbugi.
Amesema majengo yanayotarajiwa kujengwa katika Kampasi ya Mloganzila ni kumbi za mihadhara zenye uwezo kuchukuwa wanafunzi 1,400, jengo la utawala lenye uwezo wa kupokea watumiaji wa ofisi 450 kwa wakati mmoja, jengo la maktaba na Tehama litakalochukuwa watumiaji 550, jengo la maabara lenye maabara za kufundishia 21, na bweni la wanafunzi 320, bwalo la chakula lenye watumiaji 550, pia wamejipanga kutengeza uwanja wa michezo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) , Profesa Appolinary Kamuhabwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha za utekelezaji wa mradi huo.
Pia amezishukuru taasisi za JKCI, MOI na Hospitali ya Muhimbili kwa kuendelea kushirikiana na Muhas kutoa mafunzo wa wanafunzi, na kuongeza kuwa ni imani yake kwamba wataendelea kushirikiana.
Akizungumzia kuhusu wakandarasi wa mradi huo, Prof Kamuhabwa amewataka wakandarasi hao kushiriana na chuo hicho ili kutatua changamoto yoyote endapo itajitokeza.
“Najua huu mradi utaeleta ajira, maana kuna watu wataajiriwa, tuombe tuwe walinzi wa miundombinu hii, unavyoona kuna mtu anataka kuharibu tafadhari toa taarifa,” Prof Kamuhabwa amesema.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Muhas, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wakandarasi walioingia mkataba ujenzi wa miradi hiyo kuonesha thamani halisi ya fedha na ubora wa miradi hiyo.
“Mmepatikana kutokana na uwezo wenu, na rekodi yenu iliyotukuka katika sekta ya ujenzi,” amesema Dk Mwakyembe.