Serikali ya DRC yathibitisha uwepo wa Rwanda Goma

GOMA : SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imethibitisha leo kuwa jeshi la Rwanda linahusika katika mapigano yanayoendelea huko Goma, ambako waasi wa M23 wanadai kuteka mji huo.
Msemaji wa serikali ya Congo, Patrick Muyaya, amesema vikosi vya DRC vinapambana kwa bidii ili kuzuia machafuko na mauaji, huku akitoa wito kwa wakazi wa Goma kusalia majumbani mwao na kuepuka vitendo vya uharibifu wa mali na uporaji.
Mapema leo, waasi wa M23 walivamia katikati ya mji wa Goma, ambapo hali bado ni tete na maelfu ya wafungwa wanaripotiwa kutoroka kutoka gereza moja la mji huo.
Jeshi la Congo lililopo kwenye mlima wa Goma limekuwa likirusha makombora kuelekea Rwanda. SOMA:CONGO: Serikali kuimarisha usalama Goma
Msemaji wa jeshi la Rwanda, Ronald Rwivanga, amesema kuwa raia watano wa Rwanda wameuawa na wengine 25 wamejeruhiwa vibaya katika mji wa Rubavu, huko Gisenyi, ambao upo karibu na Congo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean Noel Barrot, ameelaani vikali uvamizi wa M23 huko Goma, akisema:
“Barani Afrika, katika eneo la Maziwa Makuu, mapigano yanazidi kuongezeka. Goma inajiandaa kutekwa,” alisema Barrot.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ufaransa imesema mapigano hayo yanaungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda na yamepelekea vifo vya walinda amani sita huku maelfu ya raia wakilazimika kuyahama makazi yao.
Juhudi za kimataifa na kikanda za kutafuta suluhu ya mzozo huu zinaendelea. Jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilijadili hali hiyo, huku mkutano wa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukitarajiwa kufanyika Jumatano ijayo.



