Serikali ya Rais Samia yaleta Mapinduzi Chamwino

CHAMWINO, Dodoma – Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa ya kubadili hali ya Chamwino kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba wananchi wa eneo hilo, wakiwa mashahidi wa maendeleo makubwa yaliyotekelezwa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano (2020-2025) wilayani Chamwino. Taarifa hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Chamwino, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Deogratius Ndejembi.
“Nimemsikiliza Mhe. Ndejembi akieleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa hapa Chamwino, na ni dhahiri kwamba Serikali ya CCM chini ya Rais Samia imefanya kazi kubwa katika kuboresha maisha ya wananchi na kutatua changamoto zao,” alisema Dk. Biteko, akiwapongeza wananchi wa Chamwino kwa ushirikiano wao.
Dk. Biteko alisisitiza kuwa wananchi wa Chamwino wanapaswa kuendelea kuisimamia Serikali kuanzia ngazi ya chini ili kuhakikisha kuwa maendeleo yanaendelea kugusa kila nyumba na kutatua changamoto zinazoendelea.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana na ya kipekee kuiletea nchi yetu maendeleo. Ninyi hapa Chamwino ni mashahidi wa maendeleo yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,” aliongeza Dk. Biteko.
Serikali pia imewekeza zaidi ya bilioni 13 katika sekta ya elimu ya sekondari wilayani Chamwino, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za elimu kwa wananchi.
“Tunaona maendeleo makubwa katika ujenzi wa Shule ya Mkoa ya Sekondari ya Bweni ya Wasichana ya Manchali, ambayo itahudumia Watanzania wote,” alieleza Dk. Biteko.
Aidha, serikali imewekeza zaidi ya bilioni 17.9 katika kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, na vivuko katika Jimbo la Chamwino, hatua ambayo imerahisisha usafiri na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa, aliwahimiza wakazi wa Chamwino kuendeleza umoja na mshikamano wao ili kuhakikisha maendeleo haya yanaendelea kudumu na kuongezeka.
Alhaji Kimbisa pia aliwasisitiza wakazi wa Chamwino kutumia mvua za msimu kwa kilimo cha wingi na kuhifadhi sehemu ya mavuno yao kwa ajili ya akiba ya chakula kwa siku zijazo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, alisisitiza kuwa jitihada za Rais Samia kutoa fedha za miradi zimeharakisha maendeleo katika jimbo hilo, ikiwemo usambazaji wa umeme kwa vijiji vyote.
“Kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, kata zote 14 na vijiji 47 vya Chamwino vimeunganishwa na umeme, jambo ambalo linaboresha maisha ya wananchi,” alifafanua Ndejembi.
Kwa ujumla, chini ya uongozi wa Rais Samia, Chamwino imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali, na maendeleo hayo yanaendelea kubadilisha maisha ya wananchi na kufungua milango ya fursa mpya.



