Serikali yaeleza manufaa umeme wa nje

SERIKALI imesema nchi ina umeme wa kutosha lakini itanunua megawati 100 nchini Ethiopia kwa ajili ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Imesema kununua na kuuziana umeme kwa nchi si jambo geni na Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikiununua uganda kwa ajili ya Mkoa wa Kagera, nchini Zambia kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa na Kenya kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Tanga hususani yaliyoko mpakani.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema pia ununuzi wa umeme kutoka nchi jirani haumaanishi kwamba nchi iko katika changamoto ya upungufu wa nishati hiyo kwa kuwa mpaka sasa Tanzania inazalisha umeme wa kutosha ambao ni takribani megawati 3,796.
Mramba alisema uamuzi huo una faida kwa pande zote mbili kwa kuwa njia itakayotumiwa kununua umeme nchini Ethiopia ndiyo itatumika kuuza kwa nchi zenye uhitaji.
Alisema umeme wa Ethiopia utaingizwa kwenye mfumo wa Gridi ya Kenya na kisha utaletwa nchini kufidia ulioingizwa kutoka nchini Ethiopia.
“Makubaliano hayo yako ya pande mbili, kuna wakati sisi tutanunua umeme na kuna wakati tutatumia njia hiyo hiyo kuuza umeme kwa nchi jirani, tunavyoangalia hali ya Kaskazini kwa sasa tunaona sisi tutachukua zaidi kuliko kupeleka lakini kuna wakati na wenyewe wanaweza wakahitaji umeme na tutatumia njia hiyo hiyo kuwapelekea,” alisema Mramba.
Alisema Tanzania inaendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Zambia na kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa nchi kuuza umeme kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
Mramba aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa umeme utanunuliwa kupitia Namanga na akabainisha kuwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, gridi ya taifa ni dhaifu na mara nyingi
inaposumbua au kuzima, huanzia mikoa hiyo.
“Mikoa ya kaskazini ina changamoto ya msongo kushuka na kuwa chini kuliko kawaida, hivyo kunapokuwa na shida hiyo ndipo utakuta wananchi wanalalamika kutokana na umeme kuwa mdogo na baadhi ya vitu vitaungua, kumbuka umeme upo lakini ‘voltage’ ziko chini,” alisema Mramba.
Aliongeza: “Sababu kubwa inayosababisha mikoa hiyo kupata shida hii ni kutokana na udhaifu wa gridi na ndio maana tunasema umeme utakaoingizwa pale itakuwa ni tiba ya tatizo linalosumbua kwa sasa.”
Mramba alisema chanzo cha msongo hushuka katika maeneo hayo kutokana na umbali mrefu kuanzia umeme
unapotoka hadi kwa mtumiaji.
“Kwa Tanzania, umeme unazalishwa Kanda ya Kusini, Dar es Salaam Morogoro, Pwani na Iringa hivyo mteja kama yupo mikoa ya kaskazini ni lazima umeme utoke sehemu zinazozalisha mpaka mikoa husika,” alisema.
Aliongeza: “Mfano ukituma megawati 100 kuanzia Chalinze kwenda Arusha hadi kufika kule, zitakuwa pungufu ya zile ulizotuma. Katika hatua hii ni megawati 17 za umeme ambazo zinapotea hivyo basi ili kutatua hili ni lazima kuweka mitambo ya kuzalisha umeme kule pamoja na kuingiza umeme kutoka nje ya nchi.”
Mramba alisema kuchukua umeme Ethiopia ni faida kubwa kwa nchi kwa sababu umeme huo unanunuliwa kwa bei ndogo. Kuhusu Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ambalo mpaka sasa limefikia asilimia 99.8 kabla ya kukamilika, alisema limekuwa na mchango mkubwa wa upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kule Julius Nyerere sasa hivi tunatumia umeme tunaouhitaji, kama mahitaji yetu sisi ni megawati 1,908 kwenye
Gridi ya Taifa hatuwezi kuzalisha zaidi kwa kuwa umeme utakuwa hauna matumizi,” alisema Mramba.
Awali, serikali ilisema inapata hasara ya Sh bilioni 32 kwa mwaka kwa kusafirisha umeme kuupeleka Kanda ya
Kaskazini.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu sababu za
Tanzania kupanga kununua umeme kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kanda hiyo.
Msigwa alisema umeme katika Gridi ya Taifa unazalishwa kutoka ukanda wa Kusini Mashariki na hivyo unasafirishwa umbali mrefu kwenda maeneo mbalimbali nchini hali inayosababisha upotevu mkubwa wa umeme.
“Kutokana na upotevu huo na usafirishaji mrefu wa umeme, Kanda ya Kaskazini imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kukatika kwa umeme mara kwa mara hali ambayo inawaathiri wananchi,” alisema Msigwa.
Msigwa alisema gharama za umeme unaonunuliwa Ethiopia ni nafuu kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Gridi ya Umeme ya Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika.
Alisema nchi wanachama wa gridi hiyo zimekubaliana kuuziana kwa gharama nafuu ambayo inalingana; kwa maana ni chini ya gharama za uzalishaji umeme zilizopo sasa nchi kwa baadhi ya vyanzo.
“Lengo kuu la kununua umeme kwa ajili ya maeneo ya pembezoni mwa nchi ni kuimarisha Gridi ya Taifa na
kuiwezesha nchi kuwa na njia mbadala ya kupata nishati ya umeme pale kunapotokea changamoto katika Gridi ya
Taifa,” alisema Msigwa.



