Serikali yaendelea kusambaza umeme Monduli, Karatu

SERIKALI imeendelea kusambaza umeme wilayani Monduli na Karatu ili kuhakikisha vijiji ambavyo havijafikiwa umeme vinafikiwa.

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Mto wa Mbu (Monduli) na Karatu, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango inayoendelea Arusha.

Byabato amesema katika Wilaya ya Monduli vijiji vitatu ambavyo havijafikiwa na umeme, mkandarasi anaendelea na kazi katika vijiji hivyo wakati Wilaya ya Karatu ni vijiji sita tu ambavyo pia havijafikiwa na umeme, kazi ya kuvifikishia umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili inaendelea.

Advertisement

“Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itahakikisha vijiji hivyo vinapata umeme wa uhakika ili wananchi waweze kufikiwa na huduma hiyo”.

Hata hivyo, amesema kuwa serikali imetenga jumla ya sh, bilioni 109 kwaajili ya kuendelea kusambaza umeme katika Mkoa wa Arusha, katika maeneo ya mjini na vijijini, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo uzalishaji kwenye maeneo ya Migodi, Mashamba ya Umwagiliaji na pampu za maji.