DODOMA : WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesema serikali imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 287 katika kipindi cha robo ya kwanza, ikivuka lengo la awali la makusanyo ya shilingi bilioni 247 katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa mjadala wa mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika uboreshaji wa sekta madini nchini uliofanyika kwa njia ya mtandao, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka usimamizi mzuri wa masoko ya madini ambayo imesaidia kudhibiti utoroshaji wa madini nchini .
“Masoko ya madini yamekuwa na mchango mkubwa katika kudhibiti utoroshaji wa madini na hii imesaidia kuongeza mapato ya serikali,” alisema Mavunde.
Kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, Waziri Mavunde alionyesha kuridhika na mwitikio mzuri wa wananchi kujihusisha na shughuli za madini, ambapo wengi wamechangia katika maendeleo ya jamii zao.
Aidha, Waziri Mavunde alisisitiza mikakati ya serikali katika kufanya tafiti za madini utaendelea ili kubaini maeneo mengine yenye rasilimali hizo kwa lengo la kuimarisha sekta ya madini nchini.
“Sasa hivi tunaendelea na mchakato wa kupata taarifa za madini ya kimkakati ambayo yana mahitaji makubwa duniani na tunajipanga kuwa nchi kubwa Afrika katika uzalishaji wa madini haya,” alisema Mavunde.
Kwa sasa nchi zinazoongoza katika uzalishaji wa madini ya grafiti barani Afrika ni Madagascar, inayochangia asilimia 13, Msumbiji asilimia 10, na Tanzania ikiwa na asilimia 0.6.
“Tuna miradi mikubwa 12 ya madini ya kimkakati, na tukiweza kuitekeleza, Tanzania itakuwa kiongozi katika uzalishaji wa madini haya,” aliongeza Mavunde.
Waziri Mavunde alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea na jitihada za kuongeza thamani ya uzalishaji wa madini ya kimkakati nchini, hatua itakayosaidia kuimarisha makusanyo ya mapato.