PROFESA Mshiriki wa Maendeleo ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof Abel Kinyondo ameishauri Serikali kutoa taarifa sahihi kuhusu eneo husika yanapopatikana madini katika ardhi huku ikisisitiza kuwekwa sheria rafiki na nyepesi kwa wachimbaji wadogo badala ya sheria ya jumla iliyopo sasa.
Akizungumza leo wakati wa mjadala wa mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika uboreshaji wa sekta madini nchini uliofanyika kwa njia ya mtandao, Prof Kinyondo amesema ni muhimu wachimbaji wadogo wakashirikishwa katika kuongeza thamani ya madini.
“Taarifa za kijiolojia nimesikia tu juzi Rais amesema atawekeza fedha sio kwamba hatuna taarifa ila tuna taarifa ambazo ziko jumla sana, leo hii tunaweza kusema kwamba ukienda Geita kuna madini lakini hatujafikia ule usahihi wa kusema ni wapi nitachimba na nitapata.

Ameongeza: “Ukipata taarifa ambazo ziko sahihi kiasi hicho unaweza kupata kokote pale wala huhitaji kwenda kubembeleza benki.”
Amesema wachimbaji wadogo wako milioni 6 na ni asilimia 40 ya uchimbaji uliopo mchango unatoka kwa wachimbaji wadogo hasa kwenye dhahabu.
SOMA: Mavunde aguswa na kilio cha wachimbaji wadogo
Amefafanua kuwa miongoni mwa sababu za mchango huo ni kuwepo kwa masoko ikiwemo masoko takribani 43, vituo vya uuzaji zaidi ya 100 na vituo vya umahiri vya watu kupata mafunzo.
“Ukienda kwenye maeneo utashangaa watu wengi wenye leseni wala hawashiriki katika uchimbaji utakuta kuna mtu anajitolea kutoa maji, mwingine umeme, chakula, mwingine kuchimba,” amesema.
Prof Kinyondo amebainisha kuwa kwenye maeneo ya uchimbaji kuna changamoto ya utunzaji wa mazingira na afya ambapo wachimbaji hawana uelewa wa kutosha hivyo elimu inahitajika.
“Nilikuwa Chunya muda si mrefu wakati tunazungumza kuachana na mekyuri ambayo inaathari kwa binadamu na kuanza kutumia madini mengi safi kwa mazingira na binadamu, nilikuta mtu aliyekuwa pale muda mrefu ananipa ushuhuda kwamba mekyuri haina shida anachukua maji yenye Mekyuri halafu anakunywa nikamwabia unajua ni hatari? akaniambia hapana hii ukiwa tu na vidonda vya tumbo inasumbua,”anaeleza Prof Kinyondo.
Akizungumza kuhusu sheria zilizopo Prof Kinyondo amesema zina muunganiko wa moja kwa moja wa sheria za madini kwa ujumla huku namna uchimbaji mdogo unafanyika ni tofauti na uchimbaji mkubwa hivyo kunapokuwa na sheria moja kuna kitu kinakosekana.
“Natamani uchimbaji mdogo uangaliwe kwa namna yake ya tofauti yule ambaye chukua leseni mara nyingi sio wanaochimba kuna mjumuiko wa watu wengi tutaweza kuwajumlisha hawa wote kuwe na sheria ya kwamba waone umuhimu wa mazingira, afya zao kwa namna ya viwango vizuri.
Aidha amesema thamani ya madini inahitaji kuongezwa kulingana na mahitaji ya dunia ya sasa hadi kwa wachimbaji wadogo huku mkazo mkubwa wa kujifunza ukiwekwa kutoka nchi zilizofanikiwa kama za bara la Asia.
“Kule watu wanaoongeza thamani sio wanajiolojia wamerithishana vizazi hadi vizazi na hapa kwetu watu hawana vigezo sasa tuondokane na sheria zetu za kazi zilizopitwa na wakati.
Comments are closed.