Mavunde aguswa na kilio cha wachimbaji wadogo

MANYARA: SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imesema inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara na ina mipango ya muda mrefu na muda mfupi wa kuzitatua changamoto hizo.

Hayo yamebainishwa  na Waziri wa Madini Anthony Mavunde  wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa Madini ya Tanzanite, wafanyabiashara na wamiliki wa vitalu vya uchimbaji madini katika mkutano maalum ulioitishwa na Serikali ili kujadili changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

Advertisement

Mapema baada ya Mkuu wa Mkoa wa  Manyara Queen Sendiga kutoa taarifa , wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya Tanzanite walielezea juu ya changamoto walizonazo ikiwa pamoja na ukosefu wa Nishati ya Umeme katika migodi , mitobozano chini ya ardhi , ubovu wa miundombinu ya Barabara, kukosekana kwa minada ya kuuza madini , ukosefu wa maji na vituo vya afya, ukosefu wa mitaji ya kuendeleza uchimbaji na vifaa duni vya uchimbaji.

Akielezea kuhusu mikakati iliyopo ya kutatua changamoto hizo Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupitia upya kanuni za masoko, uongezaji thamani na kanuni za  eneo tengefu la Mererani ili kufanikisha minada ya vito pasipo vikwazo.

Kuhusu Mitobozano, Mavunde amesema hakuna sheria inayoruhusu mitobozano katika uchimbaji madini kisheria leseni zote zina mipaka hivyo kila mchimbaji azingatie mipaka yake iliyopo katika leseni na kumtaka Afisa Madini Mkazi wa Mirerani kuhakiksha anakaa na wadau kutatua changamoto ili kuruhusu shughuli za madini ziendelee pasipo kuleta athari katika ukuaji wa sekta.

Akijibu hoja ya kuwepo kwa zahanati  katika mgodi , Mavunde ameeleza kuwa mpango wa Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ni kujenga  zahanati 11  katika Wilaya ya Simanjiro na zahanati moja  itajengwa ndani ya mgodi ili wachimbaji waweze kupata huduma ya haraka.

Akifafanua kuhusu uwezeshwaji wa mitaji na vifaa vya kufanyia kazi , Waziri Mavunde amesema tayari timu maalum imeishakaa na taasisi za fedha na Benki kuangalia namna bora ya kutoa mikopo kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini na kwasasa yapo maeneo ambayo wameanza kunufaika na mkopo huu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga  amemtaka Meneja wa TANESCO Wilaya ya Simanjiro ifikapo siku ya  jumatatu kupeleka mpango kazi wa usambazaji  umeme katika maeneo yanayohitaji huduma hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo sehemu kubwa ya nishati ya  umeme ipo katika eneo ambalo kwa sasa bado hawaitaji huduma hiyo.

 

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *