Serikali yaita tril 11/- uwekezaji nishati

SERIKALI imesema imefungua dirisha ili sekta binafsi iwekeze dola za Marekani bilioni nne (zaidi ya Sh trilioni 10.78) katika sekta ya nishati.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Upokeaji na Uhifadhi wa Nishati Safi ya Kupikia wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 100 (zaidi ya Sh bilioni 269.7) katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga.

Mradi huo unatekelezwa kwa ubia wa kampuni tanzu ya ASAS za Tanzania kwa ushirikiano na kampuni ya kigeni ya Petredec.

Dk Biteko alisema uwekezaji katika sekta binafsi kwenye sekta ya nishati nchini haujawahi kuzidi zaidi ya Dola za Marekani milioni 500 hivyo mradi huo unafungua milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wazawa na wageni.

“Mkiona ndugu zetu hawa wamekuja ni kwamba serikali imetoa fursa kwa kila mwenye uhitaji wa kufanya uwekezaji kwenye sekta hiyo kutoka nje ya nchi au ndani kuja kufanya uwekezaji hapa nchini kwa ajili ya kupata faida yeye na nchi kwa ujumla,” alisema Dk Biteko.

Aliongeza: “Katika uwekezaji wa dola bilioni nne ambazo serikali imetenga kwa ajili ya uwekezaji huo, tayari tumeshapata milioni 100 na sasa tunatafuta bilioni 3.9 kwa ajili ya wawekezaji wengine ambao tayari  ameonyesha nia ya kuja kuwekeza kwenye sekta ya nishati, umeme na mafuta sambamba na miundombinu mbalimbali”.

Dk Biteko alisema matumizi ya gesi ya kupikia nchini yameendelea kuongezeka kwa kasi ya zaidi ya asilimia 38 katika miaka ya hivi karibuni kutoka mwaka 2023/2024, yameweza kufikia tani 403,000 ikilinganishwa na tani 293,000 kwa mwaka 2022/2023.

“Ongezeko hilo limetokana na kampeni yetu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ambayo imekuwa ikitiliwa nguvu ya maono mapana ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan,” alieleza Naibu Waziri Mkuu.

Alisema ujio wa mradi huo unatokana na mwitikio wa kampeni hiyo na utakapokamilika utaongeza kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi ya kupikia sambamba na kupunguza gharama ya nishati hiyo.

“Kwa sasa ukuaji wa nishati safi ya kupikia umetoka katika asilimia sita ambayo tulikuwa nayo kabla ya mwaka 2022 na sasa imeweza kufikia asilimia 16 toka tulipoanzisha kampeni hiyo. Niwahakikishie wawekezaji kuwa kuna soko kubwa la nishati ya kupikia hapa nchini,” alieleza Dk Biteko.

Dk Biteko alisema mpaka sasa serikali kupitia miradi ya Wakala ya Umeme Vijijini (REA) imetoa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku zaidi ya mitungi 452,450 na hadi kufikia Aprili, mwaka huu tayari mitungi 154,224  imesambazwa nchi nzima.

Amewaagiza wawekezaji wa mradi huo kuwatumia wazawa katika kazi ambazo hazitahitaji utaalamu badala ya kutoa wageni kutoka nje ya nchini ili kutengeneza fursa ya ajira kwa wazawa.

“Tuangalie utaratibu katika ujenzi wa mradi huu kwani hatuna sababu ya kutafuta kampuni kutoka mbali wakati wapo Watanzania wenye uwezo wa kufanya hizo kazi,” alisema Dk Biteko.

Mwekezaji mzawa katika mradi huo Kampuni ya Asas, Ahmed Abri alisema mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira 320 wakati wa ujenzi wake na baada ya kuanza kazi jumla ya ajira 2,000 zitawanufaisha wakazi wa Tanga na mikoa ya jirani.

Ahmed alisema mradi huo utakuwa na uwezo wa kupokea gesi yenye ujazo wa lita 45,000 na mahitaji ya nchi ikiwa ni lita za ujazo 18,000 pekee.

“Mradi huu unakwenda kuifungua Tanga kimataifa kwani hata nchi za jirani kama vile Kenya, Uganda na Congo zitaweza kutumia kituo hiki kuweza kuchukuwa nishati hiyo,” alieleza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button