Serikali yaita wawekezaji ujenzi wa makazi mil 3.8
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya makazi nchini kwa sababu kuna uhitaji mkubwa wa makazi.
Ndejembi ametoa mwito huo Dar es Salaam wakati wa semina kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa sekta ya makazi kutoka Japan.
Alisema kwa sasa kuna uhitaji wa makazi milioni 3.8 kwa mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukua kwa miji.
“Ukiangalia miaka ya 1960 na 1967 ukuaji wetu katika miji ulikuwa katika asilimia 6.2 tu, lakini katika Sensa ya mwaka 2022 ukuaji wa miji umekwenda asilimia 34.9 ni ukuaji wa kasi sana,” alisema.
Ndejembi alisema tayari serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya 1995 toleo la 2025 ambayo inaruhusu uwekezaji katika sekta ya makazi ili kukabiliana na changamoto hiyo na kuhakikisha wananchi wanapata makazi kwa bei nafuu.
Vilevile alisema sambamba na jitihada hizo, pia serikali imeandaa mipango mbalimbali ikiwemo nyumba za bei nafuu za Samia ambapo mwananchi atanunua nyumba kwa bei nafuu na pamoja na kuendelea na mazungumzo na mataifa mengine kwa ajili ya kupata teknolojia mpya katika ujenzi wa makazi na kuendeleza miji na majiji nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Revocutus Rasheli alisema Tanzania imepata uwekezaji mkubwa kutoka Japan katika sekta za viwanda, nyumba na miundombinu.
“Hadi sasa tumepata uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 43 kutoka Japan, kwa hiyo hawa ni wawekezaji muhimu kutoka sekta binafsi na tumechukulia tukio hili kwa umuhimu kwa ajili ya kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo hapa Tanzania kwa Japan,” alisema.
Naye Mshauri Mtendaji, Kituo cha Ujenzi cha Japan, Dk Izumi Hiroto alisema baada ya vita kuu ya pili ya dunia hali ya makazi nchini humo ilikuwa duni lakini kutokana na jitihada ambazo zimefanyika sasa hivi kuna ziada
ya makazi milioni nane nchini humo.



