Serikali yajipanga kuzalisha nguvu kazi

SERIKALI imepongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kuandaa mkutano muhimu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), hatua inayolenga kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na kuongeza ujuzi wa nguvu kazi nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, alisema Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), inayolenga kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi, ubunifu na tija katika soko la ajira.

“Lengo ni kuhakikisha Tanzania inazalisha nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda nchini,” alisema Prof. Nombo.

Profesa Nombo alisema kuwa VETA imeendelea kuboresha mitaala, miundombinu na mbinu za ufundishaji ili kuhakikisha mafunzo yanayotoa yanakidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma. Kwa sasa, vyuo vya ufundi stadi nchini ni zaidi ya 900, huku VETA ikisimamia vyuo 80 vinavyotoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 300,000 kila mwaka.

Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kujenga vyuo vingine 64 katika wilaya mbalimbali na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe, hatua inayolenga kufikia vyuo 145 ifikapo mwaka 2026.

“Hii itawezesha wananchi kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza tija katika shughuli za kijamii na kiuchumi,” alisema Prof. Nombo.

Aidha, VETA imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kutoa mafunzo ya vitendo, ubunifu na ujasiriamali. Wanafunzi wamepata mafunzo katika makampuni makubwa ya madini kama Barrick, Geita Gold Mining na North Mara, pamoja na mahoteli ya kitalii katika miji ya Arusha, Dar es Salaam, Tanga na Moshi.

Kupitia programu ya Urasimishaji wa Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi (RPL), maelfu ya Watanzania wamefanikiwa kupata vyeti vya kitaalam, hatua iliyowawezesha kupata ajira na kuinua kipato chao. SOMA: Bil 19.1/- zatumika kujenga vyuo vya VETA 4

Prof. Nombo pia alizungumzia miradi ya kimkakati, akieleza VETA imechangia kikamilifu katika mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kutoa mafunzo maalum kwa Watanzania kushiriki katika ujenzi na usimamizi wa bomba hilo. Hadi mwaka 2024, kulikuwa na zaidi ya viwanda 8,400 vilivyosajiliwa nchini, ikiwemo zaidi ya 200 vikubwa vinavyotoa mchango mkubwa katika ajira na pato la Taifa.

“Ukuaji wa viwanda unaibua mahitaji makubwa ya nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa. Katika miaka mitano ijayo, zaidi ya ajira 700,000 mpya zitahitajika katika sekta za viwanda, nishati na ujenzi,” alisisitiza Prof. Nombo.

Profesa Nombo ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda na waajiri kufungua milango kwa vijana kupata mafunzo ya vitendo pamoja na nafasi kwa wakufunzi kupata uzoefu kupitia programu za mafunzo viwandani. Pia amewataka wadau kushirikiana na VETA kuendeleza programu za Uanagenzi Rasmi (Dual Apprenticeship Training System – DATS) zilizothibitisha mafanikio katika kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi soko la ajira.

“Viwanda vina nafasi kubwa ya kusaidia ubunifu wa wanafunzi. Fanyeni makubaliano kati ya VETA, wabunifu na viwanda ili bunifu ziwe bidhaa za kibiashara,” aliongeza.

Profesa Nombo aliagiza VETA na wadau wa sekta hiyo kuendelea kukutana angalau mara moja kwa mwaka kujadili mafanikio, changamoto na mikakati mipya ya kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. Google pays $220 an hour online. My close relative had been unemployed for nine months, but last month, she received a $25k paycheck by working from home for 10 hours a day. Everyone should try this job now—just use this link.

    COPY THIS →→→→ http://Www.Work99.Site

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button