Serikali yakamilisha upembuzi wa reli ya SGR Mtwara–Bamba Bay

DODOMA: Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kutoka Mtwara-Mbambabay pamoja na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya urefu wa kilometa 1,000.

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kujua kama Serikali haioni haja ya kuanza upembuzi wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kusini, hususan ikizingatiwa maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Gesi Asilia (LNG).

Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa, ikiwemo kutumia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

Aidha, amesema kwa upande wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara, Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia mpango kabambe wa East Africa Railway Master Plan imetambua umuhimu wa kipande hicho cha reli kitakachounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Mtwara, kutokana na mchango wake katika kukuza uchumi, maendeleo ya kijamii na kuimarisha mtangamano wa kikanda.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema reli hiyo bado haijaingizwa katika mpango wa utekelezaji kwa kutumia fedha za Serikali kwa sasa, kutokana na Serikali kuendelea na ujenzi wa reli ya SGR pamoja na utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati inayohitaji rasilimali kubwa za kifedha kwa wakati mmoja.

Kutokana na hali hiyo, Kihenzile ametoa wito kwa wawekezaji wa sekta binafsi na taasisi za kifedha kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya reli, ikiwemo reli ya kusini, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha miundombinu ya usafirishaji nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button