Serikali yaongeza msukumo wa biashara Tanzania, China

DAR ES SALAAM: Serikali imewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi nchini China ili kukuza biashara zao na kuongeza mauzo ya bidhaa za ndani nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo wakati akizindua Siku ya Huduma (Clinic Day) iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini China katika Maonesho ya Sabasaba, inayolenga kutoa taarifa za uwekezaji, utalii na elimu, Julai 04, 2026.
Amebainisha kuwa ushiriki huo wa ubalozi unadhihirisha utekelezaji wa vitendo wa Diplomasia ya Uchumi kuelekea Dira ya Taifa 2050.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia mageuzi ya kisera na kisheria katika wakati ambao China ni mshirika mkubwa wa kimkakati wa Tanzania katika viwanda, teknolojia na biashara, jambo linalotoa fursa kubwa ya maendeleo kwa wananchi.
Ameeleza kuwa, kupitia sera ya ushuru sifuri inayotolewa na China, ni wakati sasa wa kuona bidhaa nyingi zenye nembo ya ‘Made in Tanzania’ zikiingia katika soko hilo.
Katika hatua nyingine amesema Serikali itawashughulikia wote wanaoharibu taswira ya Tanzania katika sekta ya biashara.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman, amesema kupitia kliniki hiyo ubalozi huo umefanikiwa kutoa taarifa muhimu kwa Watanzania wengi wanaotaka kufanya biashara na China.



