Serikali yaonya uuzaji, usambazaji dawa bandia

SERIKALI imeonya kwamba haitamvumilia mfanyabiashara yeyote atakayeuza au kusambaza dawa bandia au vifaatiba duni kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ametoa onyo hilo wakati akifungua kikaokazi cha Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) na wahariri kwa mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Chacha alisema kuuza au kusambaza dawa na vifaatiba ni kosa na lina athari kwa jamii, hivyo serikali haitamvumilia yeyote anayesambaza vifaa dunia na zisivyo na ubora.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kujali afya za wananchi wake na imefanya mambo makubwa mazuri katika sekta ya afya, kwa hiyo haitavumilia vitendo hivi,” alisema.

Chacha aliipongeza TMDA kwa kazi inayofanya ambayo imetoa mchango katika udhibiti wa dawa na vifaatiba.

Alipongeza uwekezaji uliofanywa na Rais Samia katika sekta ya afya ikiwa ni moja ya vipaumbele vyake katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

Kuhusu wanahabari, Chacha aliwataka kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa afya na hasa kuwafichua wote ambao wanashiriki vitendo viovu na wanaopotosha wananchi kuhusu tiba kupitia matangazo ya biashara yanayotolewa na vyombo vya habari.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk Andrew Fimbo alisema katika miaka minne ya Rais Samia kumejengwa viwanda 18 vya dawa nchini vinavyotoa ajira kuanzia 100.

“Pia, katika miaka minne ya Rais Samia tumejenga maabara za kisasa za uchunguzi wa bidhaa za afya. Tuna maabara tatu kubwa za Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza,” alisema.

Dk Fimbo alisema katika miaka hiyo minne ya Awamu ya Sita wametoa gawio la Sh bilioni 23.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Honoratha Rutanisibwa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, alisema uwekezaji wa sekta ya afya mkoani humo umeongezeka kutoka Sh bilioni 4.2 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Sh bilioni 9.8 mwaka 2023/2025.

Alisema hadi Juni mwaka huu upatikanaji wa dawa mkoani Tabora ni asilimia 91.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button