Serikali yapata mafanikio mapambano dhidi ya rushwa

DAR ES SALAAM; SERIKALI ya Awamu ya Sita imepata mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kipindi cha mwaka 2023/24.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 27, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila, wakati wa kukabidhi taarifa ya utendaji kazi ya mwaka 2023/2024 kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, Ikulu, Dar es Salaam.

“Serikali ya Awamu ya Sita unayoiongoza, imepata mafanikio katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini katika kipindi cha mwaka 2023/24. Mafanikio haya yamewezesha kuimarika kwa nidhamu, uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika utumishi wa umma,” amesema.

Ametaja maeneo mengine yaliyoimarika ni uwekezaji, ukusanyaji mapato pamoja na matumizi ya fedha za umma na kwamba mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa nchini yameimarisha utawala bora; utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kufikiwa kwa thamani ya fedha kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Mheshimiwa Rais, matokeo ya mafanikio haya yamethibitishwa na taarifa inayotolewa na shirika la kimataifa la Transparency International. Taarifa ya “Transparency International” kwa kutumia kiashiria cha “the Corruption Perceptions Index (CPI)”, iliyotolewa Februari 11, 2025, imeonesha kwamba Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na kiwango cha chini zaidi cha vitendo vya rushwa kati ya nchi 10 za Jumuiya ya Afrika Mashariki,’ amesema.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa taarifa zinaonesha Tanzania ni mojawapo ya nchi nne za Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye kuzidi kuimarika katika mapambano dhidi ya rushwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button