Serikali yapunguza utegemezi wa bajeti
SERIKALI imependekeza ukomo wa Bajeti ya Serikali wa Sh trilioni 57.04 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Ukomo huo ni sawa na ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na bajeti ya Sh trilioni 50.29 mwaka 2024/2025 unaomalizika Juni 30, mwaka huu.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amewasilisha mapendekezo hayo bungeni Dodoma mbele ya Kamati ya Bunge zima iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Dk Mwigulu alisema katika mwaka huo wa fedha, bajeti ya serikali inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya Sh trilioni 40.966 na mikopo ya ndani na nje ya Sh trilioni 16.074.

Alisema mapato hayo yanajumuisha mapato ya kodi Sh trilioni 31.826, mapato yasiyo ya kodi Sh trilioni 6.234, mapato ya halmashauri Sh trilioni 1.68. na misaada Sh trilioni 1.225.
Dk Mwigulu alisema mapato ya ndani yanatarajia kugharamia asilimia 69.7 ya bajeti yote mwaka 2025/2026 ikiwa ni mkakati wa serikali wa kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyotabirika au vyenye masharti na gharama kubwa.
“Vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2025/2026 vitaendelea kuzingatia maeneo makuu ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa
viwandani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara na kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu,” alifafanua Dk Mwigulu.

Alitaja maeneo mahsusi ya vipaumbele ni ugharamiaji wa deni la serikali, mishahara, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na uimarishaji wa demokrasia nchini, kuimarisha amani, utulivu, usalama na maandalizi ya michuano ya fainali za Afrika, AFCON 2027.
“Aidha, bajeti hii itahusisha maandalizi ya nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Vilevile, bajeti ya mwaka 2025/2026 imezingatia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya sera za
washirika wa maendeleo hususani Marekani,” alibainisha Waziri wa Fedha.
Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali itaendelea kuweka kipaumbele katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutekeleza mikakati mbalimbali.

Alitaja mikakati hiyo ni kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa kuimarisha mahusiano mazuri na walipakodi, kuimarisha vyanzo vilivyopo vya mapato pamoja na kutanua wigo kwa kuibua vyanzo vipya na kuunganisha mifumo ya TRA na mifumo ya taasisi nyingine za umma.
“Aidha, serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai, kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST) ili kuendana na ubora na thamani ya fedha, na kuboresha miundombinu
wezeshi itakayovutia uwekezaji,” alisema Dk Mwigulu.
Dk Mwigulu ametangaza shabaha sita za uchumi wa jumla kwa mwaka 2025/2026 ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025 kutoka matarajio ya asilimia 5.4 mwaka 2024.



