Serikali yasitisha mikopo ya 10% halmashauri

 WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezielekeza halmashauri zisitishe utoaji wa fedha za mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu zinazotokana na makusanyo ya kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Waziri Mkuu amelieleza Bunge kuwa mikopo hiyo inasitishwa ili kuipa fursa serikali kujipanga kuwa na mfumo mpya wa kuitoa.

Alisema hayo jana wakati akihitimisha mjadala kuhusu hoja ya makadirio na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2023/2024.

Majaliwa alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wabunge kuhusu kiasi kidogo cha fedha za mikopo kinachotolewa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.

“Aidha, kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya halmashauri kutoa fedha hizo kwa watumishi wa halmashauri au wakati mwingine vikundi hewa badala ya walengwa na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa,” alisema Majaliwa.

Aliongeza: “Nazielekeza halmashauri kote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo hiyo zinazotokana na makusanyo ya kuanzia Aprili hadi Juni, 2023 wakati serikali inajipanga kuwa na mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.”

Mfuko wa Jimbo

Majaliwa amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri waheshimu na kuzingatia vipaumbele vinavyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo.

Pia amewaagiza viongozi hao wahakikishe matumizi ya fedha hizo yanazingatia Sheria ya Mfuko wa Jimbo, na Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Majaliwa pia amemwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhakikisha maofisa manunuzi kwenye halmashauri hawawi kikwazo katika utekelezaji wa vipaumbele vya matumizi ya Fedha za Mfuko wa Jimbo hususani upatikanaji wa vifaa kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Ripoti ya CAG

Alisema serikali imeanza kuifanyia kazi taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na haitamfumbia macho yeyote atakayebainika kutumia vibaya fedha na mali za umma.

Alitaja baadhi ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kuhakikisha maofisa masuuli wanaandaa majibu ya hoja kama inavyoelekezwa katika Sheria na Kanuni za Ukaguzi wa Umma na kusisitizwa na Rais Samia.

Pia amewakumbusha maofisa masuuli wazingatie maelekezo ya Rais Samia kuhakikisha wanapitia taarifa ya CAG, kujibu na kuchukua hatua za haraka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button