Serikali yatafuta wawekezaji bandari zote

KITUO cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kimesema serikali inatafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekezakatika bandari zote nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho, David Kafulila amesema wanatafuta wawekezaji wa bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa na Bandari ya Bagamoyo.
Kafulila amesema hayo kwenye Kongamano la Kitaaluma la Utekelezaji wa Uchumi Jumuishi kufikia Dira ya 2050 lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM).
Amesema kupitia ubia wamefani- kiwa kujenga reli ya kisasa inayotoka Dar es Salaam hadi Dodoma na inatarajiwa kuendelea hadi mkoani Mwanza, viwanja vya ndege, jambo linaloonesha kuwa huo ni mradi wa mapinduzi katika kufikia uchumi unaotakiwa.
SOMA: PPP nguzo ya utekelezaji Dira 2050
“Tunatafuta mwekezaji kwenye reli ili aweze kuleta vichwa vya treni na mabehewa, na anaongoza kama ambavyo serikali inajenga barabara na kuruhusu kampuni binafsi kuendesha mabasi yao. Hivyo si dhambi, ni utaratibu kisheria. Kama mwekezaji amepatikana, anaingia mkataba na serikali,” amesema Kafulila.
Ameongeza: “Ukisikia mradi wa ubia si kwamba umebinafsishwa bali ile ni ndoa lakini umiliki wa mradi unabaki kwa umma na si vinginevyo. Mfano mzuri, tulifanikiwa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam kupitia teknolojia na mtaji, jambo ambalo wengi waliamini imeuzwa kitu ambacho si kweli.”
Kafulila amesema kabla ya mwekezaji kupeleka teknolojia na mtaji kwa ajili ya kuongeza ubora wa bandari hiyo wakati serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani mwaka 2021 mzigo uliokuwa unabebwa bandarini ulikuwa ni tani milioni 17.
“Lakini tangu kuanza kwa ubia huo katika kipindi cha miaka minne inabeba zaidi ya tani milioni 30. Ni vyema kufahamu kuwa asilimia 80 ya biashara zote duniani zinafanywa kupitia bahari,” amesema.
Kafulila amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepata mafanikio kwenye sekta mbalimbali na akatoa mfano wa tija kwenye kilimo.
Amesema katika miaka minne ruzuku ya mbolea imeongezeka kutoka tani 600,000 hadi milioni 1.2 na wastani wa matumizi ya mbolea kwa hekta imeongezeka kutoka kilo 19 hadi kilo 24.
Kuhusu miundombinu ya barabara vijijini, amesema imeongezeka kutoka kilometa 108,000 hadi kufikia 144,000, sawa na ongezeko la kilometa elfu 36.
“Asilimia 25 ya barabara vijijini zimejengwa katika kipindi cha miaka minne. Hii imerahisisha shughuli za kilimo, na tayari tuna kiwanda kinachojengwa pale Dodoma kitakachokuwa kinatengeneza tani milioni moja za mbolea, hivyo kuongeza uzalishaji na kuondoa changamoto katika kilimo na mwisho kufikia uchumi unaotakiwa,” amesema Kafulila.
Amesema sekta ya umwagiliaji imepiga hatua kutoka hekta 540,000 mwaka 2021 na kufikia 980,000 kwa miaka minne.
Hivyo eneo la umwagiliaji lililotengenezwa katika kipindi hicho ni zaidi ya lililotengenezwa kwa miaka 60 kabla ya awamu ya sita.
Aidha, sekta ya uvuvi imekua kupitia mauzo ya samaki nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 kutoka bilioni 450 hadi kufikia zaidi ya bilioni 600.
“Tayari Bandari ya Kilwa, ambayo ni kubwa kuliko zote Afrika Mashariki na inayogharimu kiasi cha Sh bilioni 270, inajengwa ili biashara na uvuvi ziendelee kufanyika, kupunguza umasikini na kukuza pato la taifa,” amesema Kafulila.
Kuhusu sekta ya mifugo alisema serikali kupitia sekta binafsi imeongeza viwanda vya kuchakata nyama kutoka vitatu hadi saba.
Amesema awali sekta ya madini ilikuwa ikimilikiwa na wageni na watu wenye mitaji mikubwa ya teknolojia lakini kwa sasa hatua kubwa imefikiwa jambo linaloonesha wazi kufanikisha dira hiyo.
“Mwaka 2021 wachimbaji wadogo walikuwa wanachangia asilimia 20 ya pato la madini lakini mwaka 2024 wanachangia asilimia 40… ni wazi kasi imepigwa, na hii inajibu swali la je, tunajenga uchumi jumuishi? Ndiyo, kwa kuzipa kipaumbele sekta zin- azobeba watu wengi zaidi,” amesema Kafulila.