Serikali yatoa Sh bil 3.3 kukwamua urasimishaji Dar

ILALA, Dar es Salaam: WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kuhakikisha ifikapo Januari mwakani walau bikoni 40,000 ziwe zimesimikwa ardhini tayari kwa kuwarasimishia wananchi makazi yao ili kuondoa makazi holela nchini na kuwafanya wananchi wanufaike na makazi yao.
Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kivule, wilayani Ilala kwenye Uzinduzi wa Ukwamuaji Urasimishaji Makazi Awamu ya pili kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndejembi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Sh bilioni 3.3 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo lengo ni kufikia Juni, 2025 zaidi ya viwanja 70,000 viwe vimerasimishwa ambayo ni zaidi ya bikoni 140,000.
“Ifikapo Januari 30 nitakuja nipite uwandani mguu kwa mguu kuhakikisha bikoni 40,000 tayari zimesimikwa ardhini,” amesema Ndejembi.

Katika hatua nyingine, Ndejembi amekabidhi hati zilizokamilika kwa wananchi kadhaa jijini Dar es Salaam na kuwasihi wananchi wengine kujitokeza kupata hati zao kwa kulipa gharama ya Sh 140,000 kwa mchakato mzima.
SOMA:‘Hamasisheni umuhimu wa kuchukua hatimiliki za ardhi’
Aidha, Ndejembi amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuwa waadilifu katika kuteleza zoezi hilo ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unachukua asilimia 24 ya zoezi hilo linalotekelezwa nchi nzima.
“Wenyeviti wa Serikali za Mitaa msiende kuanzisha viwanja vingine kwa kubabanisha maeneo na kumilikisha watu wengine wasiofahamika na wakazi wa eneo husika,” ameagiza kiongozi huyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogoro amesema watahakikisha wanatoa ushirikiano ili programu hiyo ifanyike vizuri.
Akifungua hafla hiyo, Niabu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Lucy Kabyemera amesema mwenendo wa shughuli za Urasimishaji wa Makazi kitaifa kwa Awamu ya kwanza ya mwaka 2013-2023 unaonesha kuwa kufikia Oktoba, 2024 mitaa 2,217 katika jumla ya halmashauri 169 nchini zinatekeleza miradi ya urasimishaji makazi nchini ya mitaa 3,397 iliyopo nchi nzima.
“Jumla ya viwanja vya makazi 2,662,715 vimerasimishwa kati ya viwanja hivyo, upimaji wa viwanja 1,548,164 vimekamilika na kuidhinishwa,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliopokea hati zao za makazi leo, Abrahan Shaban amesema wamefurahi kwakuwa sasa mambo yamekuwa mepesi kupata hati tofauti na ilivyokuwa hapo awali.