Serikali yatoa tamko madai askari wanyamapori kunyanyasa raia

Yakiri askari kutumia nguvu kujilinda na kusababishia raia majeraha| Waathirika wapatiwa mil 1/- kila mmoja

SERIKALI imebaini kuwa hakuna tukio lolote la unyanyasaji wala udhalilishaji dhidi ya raia wakati askari wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakitekeleza majukumu yao katika kijiji cha ,wamavala huko Mbarali, Mbeya.

Akiwasilisha taarifa Bungeni Dodoma leo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amesema alikiri kuwa mnamo Mei 6, mwaka huu askari wa TANAPA wakiwa katika doria za kawaida walifika katika Kijiji cha Mwanavala na helikopta katika maeneo yaliyopo ndani ya Hifadhi ya Ruaha ikiwa ni sawasawa na km 20 ndani ya hifadhi ya mamlaka hiyo.

Alisema kuwa eneo hilo ni miongoni mwa sehemu ambazo wananchi hawaruhusiwi kuingia kwa kuwa ni karibu na Mto Ruaha ambao ni sehemu ya chanzo cha kupeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.

“Askari husika wakiwa katika doria za kawaida walibaini ujenzi wa maboma mawili mapya ya mifugo ndani ya hifadhi ya Ruaha kinyume cha Sheria,” alisema.

Alisema katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa wananchi hawa, waliongia kijinai na kinyume cha Sheria katika eneo la Hifadhi walizuia kutiwa nguvuni kwa kurusha mawe, fimbo, mishale na silaha nyingine za jadi na kusakizia mbwa askari wa Jeshi la Uhifadhi kwa lengo la kuwadhuru askari hao huku wakitumia silaha za jadi zilizorushwa zilitishia usalama wa Askari Jeshi la Uhifadhi waliokuwa katika kazi yao.

Ifuatayo ni ripoti kamili ya Waziri iliyowasilishwa bungeni leo Jumatatu, Mei 15, 2023

KAULI YA SERIKALI KUHUSU TUKIO LA WANANCHI WATANO KUJERUHIWA NA ASKARI WA TANAPA KATIKA HIFADHI YA TAIFA RUAHA, WILAYANI MBARALI, MKOA WA MBEYA Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 56 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari 2023, naomba kuchukua fursa hii kutoa taarifa fupi ya Serikali kuhusu tukio la Wananchi watano (5) katika Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya kujeruhiwa na Askari wa TANAPA tarehe 6 Mei 2023.

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa, mnamo tarehe 11 Mei, 2023 baada ya kipindi cha maswali na majibu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Bungeni, Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali aliomba Mwongozo kwa Mheshimiwa Spika akiomba Bunge lihairishe mjadala ili kujadili suala la dharura la Wananchi watano (5) katika Jimbo lake kujeruhiwa na Askari wa TANAPA. Mheshimiwa Mbunge alieleza kuwa Askari wa TANAPA walifika na helikopta katika Kijiji cha Mwanavala na kuvamia Wananchi, kuwapiga na kupora mifugo 250.

Aidha, Mheshimiwa Mbunge alilieleza Bunge kuwa Mwananchi ambaye mifugo yake iliporwa ameathirika kisaikolojia na anataka kujinyonga na kwamba ndugu, jamaa na marafiki wanafanya kazi ya kumlinda ili asijinyonge. Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa Maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda Mkoani Mbeya kuonana na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama na ile ya Wilaya ya Mbarali ili kupata undani wa suala hilo kwa hatua zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku hiyo hiyo tarehe 11 Mei, 2023 niliambatana na Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori na Kamishana wa Uhifadhi wa TANAPA kwenda Mkoani Mbeya na tarehe 12 Mei, 2023 asubuhi nilikutana na kufanya Kikao na Mheshimiwa Juma Zuberi Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ya Mkoa, Kanali Denisi Mwila, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali na Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ya Wilaya ya Mbarali na Viongozi wa Chama Tawala (CCM) Wilaya ya Mbarali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali ndugu Mary Mbwilo.

Mheshimiwa Spika, baaada ya Kikao hicho, Wajumbe wote tuliambatana kwenda Wilayani Mbarali ambapo nilianzia katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi na nilifanya Kikao na Viongozi wote niliowakuta (Mwenyeki wa Wilaya, Katibu wa Wilaya, Makatibu wote wa Kata wa Chama Cha Mapinduzi na baadae kuelekea eneo la tukio katika Kijiji cha Mwanavala.

Umbali wa kutoka Kijiji cha Mwanavala mpaka eneo la tukio lilipo tokea ni takribani KM 20. Kwa mipaka ya awali na ya sasa, maeneo haya yapo chini ya Hifadhi ya TANAPA na katika maeneo yote haya zipo BICON (VIGINGI) kubwa za TANAPA zilizowekwa na zinaonekana wazi. Tukiwa eneo la tukio tulifanya mazungumzo na baadhi ya Wananchi akiwemo Mwananchi ambaye Mheshimiwa Mbunge alieleza hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kuwa mifugo yake (Ng’ombe) 250 ilikuwa imeporwa na mbuzi Wawili (2) wameuwawa. Baada ya hapo tulifanya Mkutano wa hadhara na Wananchi, kwanza kuwapa pole kwa tukio lililoteka na vivile kupata uelewa wa pamoja kuhusiana na tukio hilo.

2 Mheshimiwa Spika, kufuatia Kikao tulichofanya na Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ya Mkoa na Wilaya, kutembela eneo la tukio, na baadae kufanya Mkutano wa hadhara wa Wananchi wa eneo husika ambao walishiriki kwa wingi wakiwemo waathirika na baadhi ya ndugu zao, pamoja na Madiwani akiwemo Diwani wa Kata husika Mheshimiwa Chuki Jeremiah Mbanjine, Mheshimiwa Michael Jeremia Makao, Diwani wa Kata ya Rujewa na Mheshimiwa UDES Nasoro Selemani, Diwani wa Kata ya Igawa, pamoja na viongozi wa Chama Tawala (CCM).

Kutokana na Vikao, Mikutano na ziara hiyo, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa yafuatayo yalibaininika:-

1. Ni kweli kuwa mnamo tarehe 6 Mei 2023 Askari wa TANAPA wakiwa katika doria za kawaida walifika katika Kijiji cha Mwanavala na helikopta katika maeneo yaliyopo ndani ya Hifadhi ya RUAHA ambapo ni sawasawa na KM 20 ndani ya hifadhi ya TANAPA kutoka ulipo mpaka, na eneo hilo ni katika maeneo ambayo Wananchi hawaruhusiwi kuingia kwa kuwa ni karibu na Mto RUAHA ambao ni sehemu ya chanzo cha kupeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Askari husika wakiwa katika doria za kawaida walibaini ujenzi wa maboma mawili mapya ya mifugo ndani ya hifadhi ya RUAHA kinyume cha Sheria;

2. Katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa, Wananchi hawa, waliongia kijinai na kinyume cha Sheria katika eneo la Hifadhi walizuia kutiwa nguvuni kwa kurusha mawe, fimbo, mishale na silaha nyingine za jadi na kusakizia mbwa askari wa Jeshi la Uhifadhi kwa lengo la kuwadhuru askari hao. Aidha, miongoni mwa silaha za jadi zilizorushwa zilitishia usalama wa Askari Jeshi la Uhifadhi waliokuwa katika kazi yao halali ya uhifadhi na kupelekea kitako cha bunduki aliyokuwa nayo askari kuvunjika. Nguvu waliyotumia askari kujilinda ilipelekea majeraha kwa Wananchi hao na askari Jeshi kulazimika kuwadhuru mbwa waliowasakizia kwa hofu ya kulinda maisha yao.

3. Baada ya mivutano hiyo Wananchi wote waliopata majeraha walipelekwa hospitali na walipatiwa matibabu ambayo yaligharamiwa na TANAPA na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Pamoja na kwamba tukio husika limetokea ndani ya hifadhi, Wizara iliona ni busara kutoa pole ya Shilingi milioni moja kwa kila mwananchi aliyeathirika na tukio hilo.

4. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe mbele ya Bunge lako tukufu kuwa eneo lilipotokea tukio hili ni karibu na eneo yalipotokea mauaji ya Askari wa Uhifadhi Ndugu Yusti Matei mwenye umri wa miaka 25 na Askari wa Wanyamapori wa Vijiji Ndugu Isaya Mwambe miaka michache iliyopita kwa kushambuliwa na wananchi waliovamia hifadhi kwa silaha za jadi. Takwimu za Wizara zinaonesha kwamba Askari wa Jeshi la Uhifadhi 15 wameuwa na wengine 51 wamejeruhiwa na Wananchi wavamizi ndani ya Hifadhi mbalimbali nchini wakiwa wanatekeleza majukumu yao. 5. Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa hakuna uthibitisho wa vitendo vya wanawake kuvuliwa nguo na Askari wa Uhifadhi kama ilivyoelezwa hapa Bungeni na Mheshimiwa Mbunge. 3 6. Mheshimiwa Spika, naomba kulithibitishia Bunge lako tukufu kwamba HAKUNA mwananchi yeyote aliyenyanyaswa kijinsia, lakini pia hakuna mifugo ya Mwananchi yeyote (Ng’ombe 250) iliyoporwa na hakuna Mbuzi waliyouwawa-iliyoporwa na hakuna taarifa ya mtu yeyote kutaka kujinyonga kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge katika Bunge lako tukufu; na 7. Mheshimiwa spika, Askari wote waliohusika na tukio hilo waliandikishwa maelezo Polisi kufuatia maelekezo ya Serikali na maelekezo yangu. Mheshimiwa Spika, kufuatia tukio liliojitokeza Wilayani Mbarali napenda kusisitiza maelekezo yangu niliyoyatoa Wilayani Mbarali kama ifutavyo: – 1.

Askari wote wa uhifadhi nchini watumie weledi wao katika kudhibiti uvamizi kwenye hifadhi badala ya kutumia nguvu kupita kiasi katika utekelezaji wa himasheria. Hii ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya Sheria ili Sheria ichukue mkondo wake;

2. Tukio la Mbarali limetokea ndani ya Hifadhi takriban KM 10 baada ya mpaka mpya wa hifadhi na KM 20 ndani ya mpaka wa zamani karibu kabisa na Mto Ruaha ambao ndio mto tegemezi unaozalisha maji yanayotegemewa katika Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo Serikali kupitia kodi za wananchi inatumia zaidi ya Trilioni 6.5 kulijenga, lakini pia ndio mto tegemezi wa maji ya kunywa lakini pia ndio chanzo cha maji katika mito mbalimbali nchini. Hii inadhihirisha kwamba wananchi hao waliingia ndani ya hifadhi kimakosa, bila kufuata taratibu za kisheria. Eneo hili halina ruhusa ya kulima wala kufuga, wala mapito ya wananchi na hii ni kwa kuzingatia hali halisi ya uwandani kama nilivyoeleza hapo juu sambamba na kulinda maeneo oevu ili mito iweze kurejesha mikondo yake ya asili ya mitiririko yake ya maji kama nilivyoeleza.

3. Mheshimiwa Spika, nimewasihi sana wananchi na ninaomba uniruhusu niendelee kuwasihi wananchi kufuata sheria na taratibu zote za maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kwa maslahi ya watanzania wote kwa ujumla wa vizazi vya leo na vizazi vya kesho. Naomba niendelee kuwasihi Waheshimiwa Wabunge mtusaidie, tusaidiane katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa maeneo haya yaliyohifadhiwa;

4. Wahifadhi wote nchini wawashirikishe viongozi wa Chama na Serikali katika kutatua migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi ikiwemo kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo; lakini watambue kwamba wananchi ni wahifadhi namba moja hivyo waboreshe mahusiano baina yao na wahifadhi wananchi na kila kiongozi wa uhifadhi katika eneo lake atapimwa kwa namna anavyoshirikiana na wananchi katika maeneo yao. Hivyo wakaimarishe mahusiano yao na wananchi na vijiji vinavyopakana na hifadhi. 5. Wahifadhi wote nchini waendelee kuimarisha doria, kuweka alama za mipaka, kuweka mabango na kulima mkuza ili kudhibiti uvamizi katika maeneo ya hifadhi kwa mustakabali wa nchi yetu ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo, kufua umeme na kilimo hususan programu za umwagiliaji. 4 6. Mheshimiwa Spika, ninaiagiza TANAPA kuanza ujenzi wa Rangers Post (kituo cha Askari wa Uhifadhi) ili kuimarisha ulinzi katika eneo la Hifadhi ya Ruaha Mheshimiwa Spika, katika kupata suluhisho la kudumu la migogoro katika hifadhi hii kongwe iliyoanzishwa mwaka 1910 iliyojulikana kwa jina la hifadhi ya Saba, mwaka 1946 ilibadilishwa jina na kuitwa RUNGWA na mwaka 1964 Mwalimu Nyerere aliporidhia iitwe RUAHA, Serikali inakusudia kumega eneo la hifadhi lenye ukubwa wa takribani hekta 34,000 ili zitumike kwa shughuli za maendeleo ya wananchi ambapo Wananchi wa Vijiji husika watajipangia mpango bora wa matumizi ya ardhi.

Aidha Serikali itaondoa ekari 900 ili zitumike kwa shughuli za malisho.
Wiki hii Serikali itakamilisha uthamini wa mali za wananchi katika baadhi ya maeneo ya Kijiji cha Mwanavala ili taratibu zingine za fidia ziendelee. Vilevile napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imekamilisha uwekaji wa vigingi katika mpaka mpya wa hifadhi ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha mchakato wa kuandaa rasimu ya Tangazo la Serikali (Government Notice – GN) jipya la Hifadhi ya Taifa Ruaha na mara taratibu husika zitakapokamilika Serikali itawasilisha Azimio Bungeni ili kupata ridhaa ya Bunge kama ilivyo kwa mujibu wa sheria na hatimaye kuwasilishwa GN hiyo kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha

Habari Zifananazo

Back to top button