Serikali yazungumzia kupanda bei za vyakula

SERIKALI imesema bei za vyakula katika nchi nyingi duniani zimepanda, lakini mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na nchi jirani za Kenya, Rwanda na Uganda.

Tanzania kiwango cha mfumuko wa bei ni asilimia 4.9 kwa mwezi Januari 2023 ikilinganishwa na asilimia 9.1 nchini Kenya, asilimia 10.4 Uganda na asilimia 21.7 nchini Rwanda kwa mwezi Januari, 2023. Aidha, katika mwaka 2022 mfumuko wa bei ulikuwa kwa wastani wa asilimia 4.3.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk, Ashatu Kijaji amesema bei ya Maharage imepanda kutoka Sh 215,193 kwa gunia la kilo 100 mwezi Februari, 2022 hadi kufikia Sh 301,297 mwezi Februari, 2023 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 40.

Akiwasilisha bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema wastani wa bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 90,330 mwezi Februari, 2022 hadi kufikia Sh 115,141 mwezi Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 27.5.

Dk Kijaji amesema wastani wa bei ya mchele kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 216,738 mwezi Februari, 2022 hadi Sh 291,819 mwezi Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 34.6.

“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake kwenye kiasi cha mavuno ya mazao muhimu ya chakula kama vile mchele, mahindi, maharage na viazi mviringo, mahitaji ya bidhaa hizo kwenye nchi jirani yamekuwa makubwa kuliko uzalishaji hivyo, kuchangia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula nchini na nchi jirani. “amesema Dk Kijaji.

Habari Zifananazo

Back to top button