Serikali yazungumzia ujenzi daraja Mto Mkondoa

DODOMa; SERIKALI imesaini mkataba na Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Mto Mkondoa.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi, aliyehoji ni lini serikali itajenga daraja katika mji wa Kilosa kuvuka Mto Mkondoa, ambalo limebomolewa na mafuriko.

“Mto Mkondoa upo kwenye barabara ya Dumila – Rudewa – Kilosa – Ulaya – Mikumi yenye urefu wa kilometa 142.3 katika eneo la Kilosa. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, tarehe 15 Mei, 2024 imesaini mkataba wa Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa daraja la Mto Mkondoa.

Advertisement

“Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi,” amesema Naibu Waziri.