Sh Bil 18 zahitajika kujenga mitaro Tabora

DODOMA: SERIKALI imesema kiasi cha Sh bilioni 18 kinahitajika kujenga mitaro mikubwa ili kukabiliana na mafuriko katika Mji wa Tabora.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Zainabu Katimba ametoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Hawa Mwaifunga aliyetaka kujua mkakati wa serikali kujenga mifereji kudhibiti mafuriko Tabora Mjini.

“Serikali imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mifereji mikubwa ya maji ya mvua katika Kata za Malolo, Mpera na Mwinyi ambazo zimekuwa zikikumbwa na mafuriko wakati wa kipindi cha mvua na kubaini kuwa Sh bilioni 18.47 zinahitajika kujenga mitaro mikubwa yenye urefu wa kilomita 25 katika Mji wa Tabora.

“Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23 kiasi cha Sh milioni 399.12 kutoka fedha za majimbo na tozo ya mafuta zilitumika kujenga sehemu ya mitaro hiyo yenye urefu wa kilomita 2.4.

“Pia katika mwaka 2023/24 kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) itajengwa mifereji mipya kwenye Barabara ya Kisarika yenye urefu wa kilomita 2.99, ambapo barabara hii inaunganisha Kata ya Mwinyi na Malolo,” amesema Naibu Waziri Katimba.

Habari Zifananazo

Back to top button