SERIKALI imesema imetoa Sh bilioni 20.52 kwa ajili ya uboreshaji wa Shirika la Ndege.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma leo, Majaliwa amesema shughuli zilizofanyika ni pamoja na kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege tano ambapo kati ya hizo, ndege moja ni aina ya Boeing 767-300F ya mizigo, ndege mbili aina ya Boeing 737-9, ndege moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400.
Amesema ndege nne kati ya hizo zinatarajiwa kuwasili nchini kabla ya Novemba, 2023 na ndege moja ya mizigo inatazamiwa kuwasili nchini hivi karibuni.
Majaliwa amesema kuwasili kwa ndege hizo kutasaidia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutanua mtandao wa safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi kama utalii, biashara na kilimo.