MKUU wa Wilaya ya Magu, Rachel Kassanda amesema katika kipindi cha Juali hadi Desemba 2023 wilaya hiyo ilipokea Sh bilioni 29.1 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za utawala, afya, elimu, maji na barabara.
DC Kassanda amesema hayo alipowasilisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Magu kilichofanyika katika ukumbi wa CCM wilayani humo.
Amesema katika sekta ya afya, halmashauri imetekeleza miradi ya Sh bilioni 2.2 ikiwa ni ujenzi wa miundombinu katika zahanati, ujenzi wa uzio katika kituo cha afya Kisesa na ununuzi wa vifaa katika vituo vya afya vya Kisesa, Kahangara, Shishani, Kabila na Lugeye.
Aidha katika sekta ya elimu DC Kassanda amesema halmashauri imeweza kutekeleza miradi yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 2.6 ikiwa ni ujenzi wa vyumba 67 vya madarasa ,
Ukamilishaji wa vyumba 15 vya madarasa , ukarabati wa vyumba vya madarasa 24 ujenzi wa nyumba 7 za walimu na ujenzi wa matundu 77 ya vyoo katika shule mbalimbali za msingi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Simon Mpandalume amewataka viongozi wa CCM Wilaya ya Magu kutangaza mazuri yanayofanywa na Mwenyekiti CCM ambaye pia ni na Rais Samia Suluhu Hassan huku akimshukuru Rais kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo Wilayani humo.
Amesema viongozi wa CCM wana kazi kubwa ya kwenda kusema kuhusu mazuri yote yanayofanywa na pamoja na kutangaza miradi yote inayotekelezwa Wilayani hapo.
“Kama tuna zahanati tukaseme zahanati zimejengwa , madarasa yamejengwa tukaseme tuwaambie wananchi ukweli wawe na taarifa hizo”. Alisema.