Sh bilioni 39.84 kuendeleza kiwanda cha sukari Mkulanzi
SERIKALI imetoa Sh bilioni 39.84 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulanzi ambao umefikia asilimia 75 mpaka sasa.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma leo, Majaliwa amesema katika kuendeleza mradi huo hekta 219 za miwa zimepandwa na kufanya ukubwa wa eneo lililopandwa miwa kufikia hekta 2,974 sawa na asilimia 83 ya lengo la kupanda hekta 3,600.
Amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa tani 50,000 za sukari kwa mwaka pindi kitakapoanza uzalishaji na hivyo kupunguza mahitaji ya kuagiza sukari nje ya nchi.