WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Kagera imepokea Sh billioni 4.641 kutoka serikalini kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa njia nne wa barabara ya kutoka Bukoba mjini hadi uwanja wa ndege.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa huo, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya wakati akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari wa Kanda ya Ziwa waliotembelea miradi mbalimbali iliyotolewa fedha na serikali.
Mhandisi Mwaikokesya alisema upanuzi huo ni utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais Philip Mpango aliyatoa mwezi March,2022 ambapo Sh billioni 4.651 zimetolewa tayari.
Mhandisi Mwaikokesya alisema upokeaji wa fedha hizo ulikuwa maalum kwaajili ya ukarabati na upanuzi wa kilomita 5.1 kwani barabara hiyo ilikuwa ni finyu na kutokea ajali mara kwa mara.
“Kwa Sasa tumeanza na upanuzi wa kipande cha kilomita moja ambapo ulianza Oktoba,2022 ikiwa
na mkandarasi anayetekeleza ni Kampuni ya Abemulo CO.Ltd na ameanza kazi na kukamilisha mwezi Oktoba,2024 na watu 25 tayari walikwisha lipwa fidia”alisema Mhandisi Mwaikokesya.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Kagera Adelina Sebastiani na Paschal Nakajumo walisema wamefurahi kufanyika upanuzi huo na wafanyabiashara waliopo kando ya barabara hiyo walipewa taarifa kabla ya miezi miwili wawe wamepisha.