Sh milioni 450 kutengeneza madawati Morogoro

HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imetenga Sh milioni 450 katika mwaka wa fedha 2023/2024 ili kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ukiwa mkakati wa kuondokana na upungufu wa madawati.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo , Ally Machela amesema hayo mbele ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro Mjini, Kichama Fikiri Juma wakati wa ziara ya kamati yake ya siasa ya wilaya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za utekelezaji wake.
Machela amelazimika kutoa maelezo hayo wakati kamati hiyo ilipotembelea shule ya msingi Lugala iliyopo kata ya Mindu ambayo alijionea upungufu mkubwa madawati na kuwafanya baadhi ya wanafunzi kukaa chini sakafu.
“Kwa mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya Sh milioni 450 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati ili kuondoa adha ya watoto kukaa chini , kwa shule za msingi tumetenga Sh milioni 250 na kwa shule za sekondari sh milioni 150 na hii yote ni kwa ajili ya kuondoa adha ya upungufu wa madawati shuleni “ amesema Machela
Amesema kwa sasa wapo katika mazungumzo na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho kinamiliki kiwanda cha kisasa cha kutengeneza samani waweze kutengeneza madawati kwa matumizi ya wanafunzi wa shule za Manispaa .
Naye Mwalimu mkuu wa shule ya Lugala, Weba Komba amesema kuwa shule hiyo wenye wanafunzi 881 ina madawati 150 na upungufu ni 121 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba .
Mwalimu Komba amesema shule hiyo ilianzishwa kwa nguvu za wananchi na baadaye uongozi wa halmashauri ukaongeza fedha za kumalizia ujenzi hiyo ambayo kwa sasa inatumika .
Mmoja wa mzazi wa mwanafunzi wa shule hiyo, Agnes Chitila amesema kukaa chini kwa wanafunzi hasa wa madarasa ya awali wamekuwa wakichafua nguo zao hali inayowalazimu wazazi kutumia kiasi kikubwa cha fedha kununua maji ya kufulia nguo za zao kila siku .
“Mtoto akirudi nyumbani amechafuka kila siku ni kufuaa nguo za shule wakati maji hatuna , tununua dumu la lita ishirini Sh 500 mbali na gharama nyingine tunaomba halmashauri iwatengenezee madawati.“ amesema Chitila