Sh milioni 646 kuboresha shule, hospitali Ubungo

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam, imetiliana saini makubaliano ya Sh milioni 646 na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule na hospitali katika halmashauri hiyo.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Rais wa Kanisa hilo, Juventenious Rubona amesema hiyo ni awamu ya pili baada ya kukamilisha ya kwanza, ambapo katika awamu hii watajenga miundombinu mbalimbali katika Zahanati ya Makuburi.

Amesema katika zahanati hiyo watajenga njia za kupita wagonjwa, kichomea taka, tanki la maji, mashine ya maji taka pamoja na shimo la kuhifadhi taka.

“Katika utekelezaji wa mradi huu wa Zahanati ya Makuburi Sh milioni 206 zitatumika,” amesema.

Pia amesema sh milioni 440 zitaendeleza kituo cha afya Kimara kwa kujenga ghorofa ya pili, kuweka mfumo wa umeme na maji.

“Bado tutakuwa na miradi endelevu ambapo tutafanya ukarabati shule ya msingi Msewe, kwa kukarabati madarasa tisa na matatu yatajengwa upya.

“Kibamba tutamalizia ukarabati wa madarasa, na shule ya Amani na Kawawa vivyo hivyo,” amesema.

Ameomba wakandarasi wa Halmashauri hiyo kusimamia ubora kwa kuwa hizo ni zaka za waumini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ubungo, Elias Ntiruhungwa ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa kwa kueleza kuwa bado wana uhitaji mkubwa wa miundombinu.

“Mwaka jana wanafunzi 5017 walimaliza kidato cha nne. Wanaoanza sekondari kidato cha kwanza wiki ijayo wapo 16,237.

“Kwa hiyo kuna tofauti wale walioondoka wameacha viti 5017. Kuna tofauti ya viti 11,000 vinavyotakiwa kutengenezwa. Kama halmashauri tunapambana kuhakikisha hayo yamewezekana. Mashirika ya dini kama ninyi mnakuwa mnatutua mzigo,” amesema.

Kwa upande wake meya wa halmashauri hiyo, Jaffary Nyaigesha ameshukuru kanisa hilo kwa msaada walioutoa.

Amesema mradi huo unaotekelezwa na kanisa. utaisaidia jamii kwa kupunguza msongamano kwa kiasi kikubwa katika hospitali zinakazofikiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button