Shemdoe ataka miradi inayozunguka uwanja AFCON ituzwe

ARUSHA: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Professa Riziki Shemdoe amesema kuwa fedha za mradi wa Sh bilioni 82.5 za ujenzi wa miundombinu ya barabara inayozunguka uwanja wa mpira utakaocheza mashindano ya Afrika (AFCON) ni fedha za mapato ya ndani hivyo wananchi wa Mkoa wa Arusha wametakiwa kuitunza miundombinu hiyo.

Professa Shemdoe amesema hayo leo jijini Arusha wakati wa utiaji saini kati ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) na mkandarasi wa mradi huo kampuni ya CRJE ya nchini China, shughuli iliyofanyika eneo la karibu ya uwanja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama, serikali, viongozi wa dini na wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla.

Amesema mashindano ya AFCON ni mashindano muhimu sana Afrika na yanaangaliwa na mamia ya watu wengi duniani, hivyo basi miundombinu yake ya kuzunguka uwanja huo inapaswa kuwa yenye ubora mzuri wenye kuwavutia watu wote watakaokwenda kuangalia mashindano hayo, na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia utolewaji wa fedha hizo kutoka mapato ya ndani.

Waziri amesema kutokana na umuhimu ulionyeshwa na Rais wa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu inayozunguka uwanja huo, wananchi wote wa Mkoa wa Arusha wanapaswa kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwa maslahi ya umma, na mradi huo unapaswa kukamilika mapema mwezi Mei mwakani na kusiwe na visingizio.

Amesema viongozi wa chama, serikali na wananchi wa Mkoa wa Arusha wanapaswa kumshukuru Rais kwa kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo ambao kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 75, na pia kutoa fedha nyingine kwa ajili ya miundombinu ya barabara inayozunguka uwanja huo, kwani uamuzi huo unapaswa kupongezwa na kila mmoja.

Naye Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seif amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuelekea na kuzunguka uwanja huo umegharimu kiasi hicho cha fedha na unahusisha barabara ya kilomita 19.9 ambayo itakuwa na njia nne na mbili kuingia katika maeneo ya uwanja huo kutoka barabara kuu ya Arusha–Babati.

Mhandisi Seif amesema kuwa ujenzi wa uwanja umefikia zaidi ya asilimia 75 sambamba na ujenzi wa miundombinu muhimu yenye umbali wa zaidi ya kilomita 19.9 kwa kiwango cha lami kuelekea kwenye uwanja huo kutokea barabara kuu ya Arusha–Babati na Arusha Bypass na kuzunguka uwanja huo Mateves–Bondeni kilomita 6.5, kilomita 1.5 njia nne na kilomita 5 njia mbili kutoka barabara kuu Arusha–Babati, barabara ya Lendita kilomita 2.75 njia nne, barabara ya Esseri kilomita 2.45 njia nne zote kutoka barabara kuu ya Arusha Bypass na kilomita 1.5 barabara kuzunguka uwanja.

Amesema baada ya mchakato wa ununuzi kukamilika, kampuni ya M/s China Railway Construction Engineering Group kushinda zabuni na kupewa kazi hiyo ya ujenzi wa barabara kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 82.5 kwa muda wa miezi 13, na kazi inapaswa kuanza Aprili mosi mwaka huu, huku usimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo ukifanywa na kampuni ya M/s Afrisa Consulting ya jijini Dar es Salaam kwa mkataba wenye thamani ya Sh bilioni 1.4.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni, Paul Makonda amesema kuwa Jiji la Arusha lina kiu kubwa ya barabara za lami kwani ni jiji la mwisho kuwa na barabara za lami, wakati majiji yote Tanzania yana barabara za lami, hivyo aliiomba TARURA kuhakikisha inafanya kila jitihada kutekeleza ahadi zake za ujenzi wa barabara za kiwango cha lami ili wananchi waweze kupita wakati wote.

Makonda alimshukuru Rais kwa uamuzi wake wa kuridhia kutoa fedha shilingi bilioni 82.5 kwa ajili ya miundombinu ya kuzunguka uwanja wa AFCON na kusema kuwa uamuzi huo unapaswa kupongezwa, huku akiwataka wakazi wa Arusha kushukuru kwa hilo na kuwasihi wananchi watakaolipwa fidia kupokea fedha hizo bila kuleta manung’uniko.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla ameahidi kuwasimamia wakandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya kuzunguka uwanja huo ili waweze kuimaliza kwa wakati, na kuwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pindi mkandarasi atakapoonekana anafanya kazi kwa kusuasua katika kutekeleza majukumu yake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button