Sheria kali kudhibiti ajali barabarani yaja

Sheria kali kudhibiti ajali barabarani yaja

SERIKALI imebainisha kuwa sheria kali ya usalama barabarani, itakayodhibiti ajali barabarani iko katika hatua ya mwisho kukamilika na inatarajiwa kuwasilishwa katika vikao vya Bunge vijavyo ili ijadiliwe na kupitishwa.

Pia, imesisitiza kuwa bado haijawashindwa madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda kutokana na wengi wao kutozingatia sheria za barabarani, ndio maana Jeshi la Polisi linawapatia mafunzo kwa makundi na watakaokamatwa wakivunja sheria watachukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yalielezwa bungeni Dodoma jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Masaburi (CCM).

Advertisement

Katika maswali yake ya nyongeza, mbunge huyo alitaka kujua lini serikali itatunga sheria kali ili kudhibiti ajali za barabarani na kuokoa maisha ya watu.

“Lakini pia, inaonekana kama mmeshindwa kuwadhibiti hawa bodaboda kwani wanaendelea kuendesha bila kujali sheria za barabarani wanapita hadi kwenye taa nyekundu,” alisema.

Akijibu maswali hayo, Sagini alisema tayari mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani yalishawasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni na inatarajiwa katika mabunge yajayo muswada utawasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa.

Alieleza kuwa mabadiliko ya sheria hiyo yaliyozingatia kuweka sheria kali za udhibiti wa ajali, yako katika hatua za mwisho.

Kuhusu bodaboda, Naibu waziri huyo alisema serikali haijawashindwa na tayari imeanza kuchukua hatua kwa Jeshi la Polisi kutoa mafunzo kwa makundi ya bodaboda hao ili wafahamu vyema masuala ya usalama barabarani.

“Pia, wale wanaokiuka sheria hizi hatua zimekuwa zikichukuliwa ndio maana hata kwenye vituo vyetu vya polisi kuna idadi kubwa ya pikipiki zinashikiliwa kwa makosa ya usalama barabarani,” alifafanua.

Awali, katika swali lake la msingi, Janeth alitaka kujua kama serikali haioni haja ya kuwapeleka maofisa wa usalama barabarani nchi za nje kama Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam kujifunza jinsi ya kudhibiti ajali za barabarani.

Akijibu swali hilo, Sagini alisema serikali inao utaratibu wa kutoa mafunzo kwa maofisa wa polisi na wa usalama barabarani ndani na nje ya nchi kujifunza namna bora ya kusimamia na kudhibiti ajali za barabarani.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2023, serikali iliwapeleka maofisa wa usalama barabarani 30 kwenye nchi 15 ambazo ni Marekani, Ujerumani, Japan, China, India, Vietnam, Australia, Switzerland, Falme za Kiarabu, Israel, Tunisia, Misri, Ghana, Rwanda na Afrika Kusini kujifunza masuala ya usalama barabarani.

Aidha, alisema mashirika ya kimataifa na wadau kama Jaica, UKAID, WFP, WHO, Latra, Tira, TRA, NIT na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani yanaendelea kufadhili na kutoa mafunzo ya usalama barabarani ili kupunguza ajali nchini.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *