SPIKA wa Bunge Dk Tulia Ackson ametangaza kuwa wabunge wamechanga kiasi cha Shilingi 5,023,000 kwa lengo la kumpongeza kijana Majaliwa Jackson aliyeshiriki kuwaokoa abiria wa ndege ya Precision Air.
Awali, Mbunge Hamisi Kigwangalla aliomba mwongozo bungeni akitaka wabunge wakatwe kiasi cha Sh 50,000 kutoka kwenye posho zao za leo kwa lengo la kumchangia kijana Majaliwa Jackson.
Ndipo Spika Dk Tulia Ackson alipojibu na kwa kutoa utaratibu wa namna ya kumchangia kijana huyo aliyefanya kitendo cha kishujaa kilichosababisha abiria 24 wa ndege ya Precision Air kuokolewa.
Aliwaagiza watumishi wa Bunge kuwaona wabunge wakati Waziri Mkuu Majaliwa akiendelea kutoa hoja ya kuahirisha Bunge hilo leo Ijumaa kwa lengo la kukusanya michango kwa ajili ya kumpongeza kijana huyo mwenye umri wa miaka 20.
Akitoa hoja ya kuahirisha Bunge leo, Dodoma, Waziri Mkuu ameendelea kumwaga sifa kwa kijana huyo, wananchi na viongozi wakuu wa serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuagiza kijana huyo aingizwe kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Awali, Spika alimtambulisha kijana huyo na kumpongeza kwa niaba ya wavuvi wenzake walioshiriki zoezi la uokoaji wa abiria wa Ndege ya Precsion iliyotumbukia Ziwa Victoria, takribani mita 100 kutoka uwanja wa Ndege wa Bukoba, Kagera.
Imeelezwa kuwa changamoto za hali ya hewa zilichangia kutokea ajali hiyo lakini Waziri Mkuu amewaeleza Wabunge kuwa taarifa kamili itatolewa baada ya vyombo husika kutoa ripoti za kitaalam.
Comments are closed.