Shule tano Kilolo zanufaika juhudi kidijitali

IRINGA: WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema kuwa Tanzania ipo katika mchakato wa mageuzi makubwa ya teknolojia, ambapo serikali imejizatiti kuhakikisha elimu ya Tehama inakuwa nyenzo muhimu ya maendeleo kwa vijana wa kitanzania hususan walioko mashuleni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maabara za kompyuta katika Shule ya Sekondari Nyalumbu, wilayani Kilolo mkoani Iringa, Waziri Silaa amesema dunia inaenda kasi kwenye mapinduzi ya kidijitali, na ni muhimu kwa taifa kuzalisha wataalamu wa Tehama ambao watashiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia hiyo.

“Serikali ya awamu ya sita haiko nyuma katika kuhamasisha matumizi ya Tehama kwenye sekta ya elimu. Hivi sasa inatoa vifaa vya Tehama na mafunzo kwa walimu, hasa katika shule za vijijini, ili kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa njia ya kidijitali kupitia mitaala, vitabu na rasilimali nyingine za kujifunzia,” amesema Silaa.

Uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa maabara za kompyuta unaofanyika katika shule tano za sekondari wilayani Kilolo, ambapo kila shule imepatiwa kompyuta 20 na vifaa vingine vya Tehama.

SOMA ZAIDI 

Silaa ataka minara ya mawasiliano ikamilike kwa wakati

Mradi huo umetokana na juhudi za Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Iringa, Ritha Kabati, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi.

Ritha Kabati alisema dhamira yake ni kuhakikisha vijana hasa wa vijijini wanapata nafasi ya kujifunza kwa kutumia teknolojia ya kisasa, jambo litakalowaandaa kuingia kwenye soko la ajira linalozidi kutawaliwa na Tehama.

“Dunia inaelekea katika uchumi wa kidijitali. Hivyo ni lazima serikali na wadau tuchukue hatua sasa kuwezesha vijana wetu, hasa walioko vijijini, kuendana na kasi hii ya mabadiliko ya kiteknolojia,” alisisitiza Kabati.

Kupitia maabara hizo, wanafunzi wanapata fursa ya kutumia kompyuta kwa kujifunza masomo yaliyohifadhiwa, kufanya mitihani ya taifa iliyopita, na kusoma vitabu vya kiada bila kulazimika kuunganishwa na mtandao wa intaneti.

Neila Patrick na Abdul Mpinga, wanafunzi wa shule ya sekondari Nyalumbu, wamesema ujio wa maabara hizo umefungua milango kwao kuielewa Tehama kwa vitendo na kuwawezesha kufanya mitihani ya vitendo kwa ufanisi zaidi tofauti na zamani, ambapo ni wanafunzi wachache tu waliopata fursa hiyo.

Katika hatua nyingine akiwa wilayani humo, Waziri Silaa alikagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Ibofye, kata ya Irole, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wa kuhakikisha maeneo yote ya vijijini yanaunganishwa na huduma za mawasiliano ya kidijitali.

Kwa hatua hizi, Tanzania inaendelea kujijengea mazingira ya kuwa taifa la kidijitali kwa kuhakikisha kizazi kipya kinafundwa, kinahamasishwa, na kinawezeshwa kutumia Tehama kama daraja la maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button