Shule ya sekondari yapigwa jeki

IRINGA; SHULE ya Sekondari ya Muhwana iliyoko Kijiji cha Magulilwa wilayani Iringa, imepata msaada wa kompyuta na mashine ya kudurufu mitihani na nyaraka zake zingine, ili kuiongezea ufanisi katika utoaji kwa wakati huduma zinazohitaji vifaa hivyo.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 6.5 umetolewa na mdau wa maendeleo wa wilaya hiyo, Sosten Mbedule ambaye ni wakili wa kujitegemea.

Kupatikana kwa mashine hizo kunamaliza changamoto ya ukosefu wa huduma ya kudurufu mitihani na nyaraka nyingine iliyokosekana katika shule hiyo kwa miaka mingi.

Akikabidhi msaada huo wakati shule hiyo ikifanya mahafali yake ya 14 ya kidato cha nne, Mbedule alisema; “Niliitikia ombi la shule la kusaidia kupatikana kwa vifaa hivi kwa kuwa mimi ni mdau wa maendeleo lakini pia ni zao la shule za kata.”

Jumla ya wanafunzi 138 kati ya 234 walioandikishwa kidato cha kwanza wamehitimu kidato cha nne huku waliobakia wakishindwa kukamilisha ndoto zao za kupata kiwango hicho cha elimu kwasababu mbalimbali ikiwemo mimba na utoro.

Akipongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, wakili huyo alisema kuiunga mkono serikali katika kuboresha elimu ni hatua muhimu na inaweza kuchangia maendeleo bora ya nchi.

“Kuchangia vifaa vya shule, vitabu, na vifaa vingine vya kujifunzia kunaweza kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia. Kazi hii haiwezi kufanywa na serikali pekee ni muhimu wadau wengine tukachangia,” alisema.

Aidha Mbedule amesikitishwa na taarifa ya idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo kushindwa kumaliza kidato cha nne, akisema kutatua tatizo hilo jitihada za pamoja kati ya serikali, jamii, na wadau wa elimu zinahitajika.

Mbedula alisema hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika elimu, kuboresha upatikanaji wa rasilimali, kutoa msaada kwa wanafunzi masikini, na kuendesha programu za kuhamasisha wanafunzi kuendelea na masomo yao.

Aliwata wanafunzi wanaokaribia kufanya mitihani yao ya kidato cha nne kuunda umoja wa kusoma, kukumbushana na kusaidiana kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha kila mmoja anapata matokeo mazuri.

Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Donald Kilundo amemshukuru Wakili Mbedule kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo shuleni hapo huku akiutaja mchango wake shuleni hapo unavyosaidia kutatua changamoto za kielimu shuleni hapo.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Marry
Marry
1 month ago

[Be Your Own Boss] Work online from home and earn over $15,000 just by doing an easy job. Last month I earned and received (vN)$20,000 from this job doing an easy part time job. j In fact, this job is so easy to do and regular income is much better than other normal office jobs where you have to deal with your boss…. 
HERE →→→→→→ http://www.smartcareer1.com

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x