Shule yenye miaka 106 yafanyiwa ukarabati

Msese amesema shule hiyo ambayo mwaka huu 2023 imefikisha miaka 106 tangu ianzishwe,  ilikuwa  na vyumba nane, lakini sasa ina  jumla ya vyumba 17 vya madarasa.

MOROGORO; Kilosa. SERIKALI imetoa Sh milioni 180 zilizotumika katika ujenzi na kukamilisha ukarabati mkubwa wa vyumba tisa vya madarasa na uwekaji umeme katika shule kongwe ya msingi ya Kilosa Town iliyoanzishwa na wakoloni mwaka 1917, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,  Lusia  Msese  amesema hayo wakati wa hafla  ya uzinduzi wa madarasa mapya tisa ya kisasa yaliyojengwa kutokana na mpango wa serikali kuboresha shule kongwe nchini.

Msese amesema shule hiyo ambayo mwaka huu 2023 imefikisha miaka 106 tangu ianzishwe,  ilikuwa  na vyumba nane, lakini sasa ina  jumla ya vyumba 17 vya madarasa.

Advertisement

Amesema kabla ya serikali kutenga fedha na kufanyika ukarabati huo mkubwa, majengo yake yalikuwa ni uchakavu, sehemu ya  paa kuvujisha maji na kuta zikiwa na nyufa nyingi.

Msese amesema  kuwa, shule hiyo ambayo kwa sasa ina wanafunzi 793 iliyokuwa na mkondo mmoja kwa kila darasa  kutokana na uchache wa vyumba vya madarasa ,  madawati  na uchakavu wa majengo yake ilisababisha hali ya utoro kwa wanafunzi.

Naye  Mbunge wa Jimbo la Kilosa , Profesa  Palamagamba Kabudi amesema, umri wa shule hiyo ni jambo la muujiza , hivyo  alipongeza  jitihada za serikali  za kukarabati vyumba tisa kwa kiwango cha kisasa.

Amesema ukarabati  madarasa hayo  tisa ni  sawa na kujenga shule mpya na  hivyo aliiomba halmashauri  kutobadili muonekano wa nje wa  madarasa ya zamani, ili kulinda historia ya shule hiyo kwa vizazi vya baadae.

“Kwa hiyo rai yangu kwa halmashauri msibadili muonekano wa majengo haya ya zamani yaliyozidi umri wa miaka 100 , kwani yanalindwa na sheria, hayatakiwi kubomolewa wala kubadili muonekano wa nje, “ amesisitiza Profesa Kabudi.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *