Shule zatakiwa kuweka kipaumbele kwenye sayansi

DAR ES SALAAM: SHULE zinazosimamiwa na Shirika la Uzalishaji Mali Nchini (SUMA JKT) chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) zimetakiwa kuhakikisha zinayapa kipaumbele masomo ya sayansi Ili kuzalisha wataalamu watakaosaidia kuendesha viwanda mbalimbali vinavyoanzishwa na shirika hilo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Tawi la Mafunzo Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) Meja Jenerali Ibrahim Mhona kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Jitegemee ambayo yameenda sambamba na harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ukarabati miundombinu ya shule hiyo .
Aidha amesisitiza umuhimu wa kusimamia vizuri maguezi na mabadiliko na kutekelezwa kwa asilimia 100 na Walimu wajitahidi kupandisha ufaulu wa wanafunzi.
Mkuu wa JKT na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Suma JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele amewaomba viongozi mbalimbali waliosoma katika shule hiyo kujitoa kwa upendo kufanikisha ukarabati huo huku Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Bigedia Jenerali Petro Ngata akiahidi kwamba SUMA JKT itailinda vyema shule kwa manufaa ya watanzania wengi zaidi.
Mkuu wa shule hiyo, Kanali Robart Kessy amesema kipindi cha miaka 50 shule imepinda katika changamoto mbalimbali lakini mafanikio ni kwamba zaidi ya watanzania elfu 49 wamehitimu katika shule hiyo na wengine ni viongozi wakuu wa katika maeneo mbalimbali serikalini na taasisi binafsi.
Maadhimisho hayo ya miaka 50 yalitanguliwa na shughuli mbalimbali zikiwemo za usafi wa soko la stilio lililopo Temeke, uchangiaji damu uliofanyika katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo na Bonanza la Michezo lilohusisha shule jirani.