Shule zisiathiri usingizi wa mtoto

KUMBE watoto wenye umri wa kuanzia miaka sita hadi 13 wanapaswa kupata usingizi kuanzia jumla ya saa kati ya tisa na saa 11!

Ukweli huu niliopata kupitia wataalamu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCD) unanifikirisha. Najiuliza, namna gani familia kwa maana ya wazazi na walezi pamoja na shule zinazingatia kanuni hii ya watoto kupata usin gizi wa kutosha.

Nawaza watoto wa shule kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba (umri unaohitaji jumla ya saa tisa hadi 11 za kulala), husu sani mkoani Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakishuhudiwa kwe nye vyombo vya usafiri wakienda shuleni kuanzia saa 10 alfajiri.

Advertisement

Baadhi ya watoto kwenye daladala au kwenye magari maalumu ya shule wamekuwa wak ishuhudiwa wakisinzia kutokana na kutolala usingizi wa kutosha nyumbani. Ina maana hata wanapofika shuleni, ni rahisi kusinzia darasani.

Mtoto anayeonekana barabarani kuanzia saa 10 au 11 alfajiri, ina maana huamka saa kumi kasoro. Unaweza kujiuliza, mbona kila eneo lina shule ya msingi na sekondari kiasi cha kutoruhusu watoto kusoma mbali na kulaz imika kuamka mapema?

Jibu ni kwamba, baadhi wana soma shule za mbali kwa sababu mbalimbali. Utashi wa wazazi huchangia hilo mathalani, kuchagua shule fulani za kupeleka watoto wao.

Kwa mfano, shule za umma zinazofundisha kwa Kiingereza mkoani Dar es Salaam, zote hupa tikana maeneo ya katikati ya mji na hupokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali yakiwamo ya pembe zoni ambao ni miongoni ambao hulazimika kuamka mapema.

Lakini pia zipo shule binafsi zilizojenga utamaduni wa magari yao kuwachukua watoto mapema sana na kulazimu watoto kukatisha usingizi.

Baadhi ya shule, zina magari machache hivyo huanza safari saa 10 alfajiri kwa lengo la kukamili sha kuwazungukia watoto katika maeneo mbalimbali kabla ya muda wa kuingia darasani kuisha.

Isome pia: Wazazi watakiwa kupeleka watoto shule

Aidha, kutokana na baadhi ya shule kuibuka na mtindo wa madarasa ya mitihani kuanza masomo mapema tofauti na muda wa kawaida, watoto wanaoishi mbali na shule hulazimika kuamka mapema zaidi wawahi masomo ya alfajiri.

Watoto hao hao ambao huamka kuwahi masomo, bado hutoka shu leni wakiwa wamechelewa. Wakati mwingine, hupewa kazi za kufanyia nyumbani ambazo zinaweza kuwa sababu mojawapo ya kuchelewa kulala.

Hata hivyo, ikiachwa watoto hawa ambao usingizi wao unaweza kuathiriwa na ratiba za shule, pia lipo kundi linalokosa kulala mape ma kutokana na wanafamilia ama kutojali au kutoelewa umuhimu wa kupata usingizi wa kutosha.

Kulingana na wataalamu, ili mtoto aamke saa 10 alfajiri anapaswa angalau awe amelala kati ya saa 12 jioni na saa 2 usiku. Tuji ulize, je, wangapi wanalala muda huo na je, wazazi, walezi, shule na jamii nzima inafahamu hilo na inazingatia? Laiti kila mtu angefahamu kwamba kulala usingizi wa kutosha kuna umuhimu mkubwa kiafya si tu kwa watoto bali pia kwa watu wazima; familia, shule na jamii kwa ujumla ingeona umuhimu wa kuzingatia saa za usingizi.

Shirikisho la Vyama vya Ma gonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) kupitia kitabu chake cha ‘Mtindo wa Maisha na Magon jwa yasiyoambukiza’, linaweka bayana faida za usingizi. Wataalamu wanaainisha zaidi umri na saa za usingizi zinazostahili si tu kwa watoto bali pia vijana na watu wazima.

Vijana wenye umri wa miaka kuanzia 14 hadi 17 wanapaswa kulala saa nane hadi kumi; watu wazima wenye umri wa miaka 18 hadi 64 wanasta hili kulala saa saba hadi tisa na wazee wenye umri wa miaka 65 na zaidi wanapaswa kulala saa saba hadi saa nane.

Wataalamu wanasema mtu akiwa amelala, ngozi hujijenga na homoni zinazohusika na msongo wa mawazo hupungua sana hivyo kufanya awe mpya anapoamka.

Kutolala vya kutosha huon geza uwezekano wa kupata na kutodhibiti magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu, unene na sonona. Kusinzia mara kwa mara hupunguza ufanisi na usalama shuleni na kazini.

Wataalamu wanashauri kila mtu ahakikishe anapata usingizi mzuri na unaotosha. Kwa hiyo wazazi, walezi na shule hawana budi kutambua kuwa watoto kutolala usingizi wa kutosha ni hatari kwa afya yao. Wanasayansi wanabaini sha kuwa kupata usingizi wa kutosha husaidia ubongo katika kutengeneza kumbukumbu na kuleta hisia nzuri.

Hata hivyo, pamoja na umuhimu huyo, bado familia na shule zimeen delea kuathiri usingizi wa mtoto. Tutafakari juu ya hili!