Silaa ataka minara ya mawasiliano ikamilike kwa wakati

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa ameuagiza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ( UCSAF),unayasimamia makampuni yote ya mawasiliano yaliyoingia mkataba kujenga minara 758 kote nchini ili kumaliza kazi kwa wakati kufikia Mei 12 mwaka huu kwa vile hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Slaa ametoa agizo hilo akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Idete, Kata ya Chanzulu Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Waziri Silaa amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 126 kwa ajili ya kupeleka huduma za mawasiliano katika kata 713 kwenye wilaya mbalimbali nchini.

Amesema serikali haitofumbia macho ucheleweshaji wa ukamilishaji wa minara hiyo kulingana na makubaliano yaliyoingiwa .

Waziri Silaa ameyataja makampuni ya mawasiliano yanayotekeleza miradi hiyo ni pamoja na Airtel, Vodacom, TTCL, Yas, na Halotel ambapo utakapokamilika unatarajia utatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi wapatao milioni 8.5.

Silaa pia amesema hadi sasa ,katika mradi wa Tanzania ya Kidigitali ,minara 304 imeongezewa nguvu kutoka teknolojia ya kizazi cha pili (2G) hadi kuwa na teknolojia ya kizazi cha tatu na nne kwa maana ya 3G na 4G na imekamilika kwa asilimia 100 .

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF,Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema jumla ya minara 420 kote nchini imekwisha kukamilika ujenzi wake ambapo ni sawa na asilimia 55 ya utekelezaji wa mradi huo.

Akielezea utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara mawasiliano vijijini ( DTP) kwa mkoa wa Morogoro , Mhandisi Mwasalyanda amesema jumla ya minara 69 itajengwa katika kata 65 zenye vijiji 169 vya wilaya saba za mkoa huo.

Mhandisi Mwasalyanda amesema kupitia miradi hiyo, wakazi wapatao 839,120 wa mkoa wa huo watapata huduma za mawasiliano yatakayofikishwa kwa ruzuku iliyotolewa na Serikali ya Sh bilioni 11.1.

Amesema kwa kata ya Chanzulu, yenye vijiji vinne kikiwemo cha Idete zaidi ya wananchi 7,000 wataondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu baada ya kukamilika ujenzi wa mnara huo.

Mhandisi Mwasalyanda amesema ujenzi wa mnara huo unatarajiwa kukamilika Aprili mosi mwaka huu ambapo wananchi wa maeneo hayo wataanza kupata huduma ya mtandao wa mawasilani ya simu na huduma nyingine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button