‘Simameni mikataba ya kiuchumi kwa maslahi ya taifa’

ARUSHA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewataka Mawakili wa Serikali kuimarisha uwezo wao katika usimamizi wa mikataba mikubwa ya kiuchumi na uwekezaji ili kulinda maslahi ya taifa, huku wakihakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mazingira bora yanayovutia wawekezaji.

Pia amesema sheria na mikataba bora ni nguzo muhimu ya ustawi wa uchumi, hivyo mawakili wa serikali wanapaswa kuwa na maarifa yanayoendana na mabadiliko ya biashara, teknolojia na jiografia ya kisiasa ili kutoa ushauri wa kisheria unaoendana na mahitaji ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.

Johari ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa Mawakili wa Serikali yanayolenga kuboresha utendaji, weledi na uwezo wao katika kutekeleza majukumu ya kisheria kwa ufanisi, huku yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kuwawezesha upya Mawakili wa Serikali kwa Uongozi wa Kimkakati wa Kisheria katika Kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.”

Amesema mafunzo hayo yatawajengea washiriki uwezo wa kufanya uchambuzi wa vihatarishi vya kisheria, kiuchumi na kisiasa ili kutoa ushauri utakaosaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Sheria na mikataba bora ni nguzo muhimu ya ustawi wa uchumi, hivyo wakili wa serikali anatakiwa kuwa na maarifa yanayokwenda sambamba na mabadiliko ya biashara, teknolojia na jiografia ya kisiasa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uratibu wa Huduma za Ushauri wa Kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Neema Ringo, amewataka Mawakili wa Serikali kutumia sheria kama nyenzo muhimu ya kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha mfumo wa sheria unaendana na malengo ya maendeleo ya nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button