MWENYEKITI wa Simba, Murtaza Mangungu amesema tayari wameanza mchakato wa kukisuka upya kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.
Simba inamaliza msimu wa pili mfululizo bila taji lolote kitendo ambacho kimewakera mashabiki na viongozi wa timu hiyo na sasa wameamua kufanya kweli kwa kukisuka upya kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu ujao.
Akizungumza na HabariLEO, Mangungu alisema wamekuwa na vikao na bodi ya wakurugenzi ya klabu na benchi la ufundi la klabu hiyo kujadili namna bora ya kupata wachezaji watakaorejesha heshima ya timu hiyo msimu ujao.
“Jambo la msingi ni kuwa tumepokea kilichotokea kama changamoto na kufanya tathmini ya wapi tumekosea na tunatarajia kufanya maboresho makubwa ya kikosi chetu, tunasubiri ripoti ya benchi la ufundi kujua ni mchezaji gani atakuwa sehemu ya mahitaji kwa msimu ujao na yupi atalazimika kuondoka.”
Simba itashiriki michuano ya Super Cup mwezi Agosti mwaka huu na Mwenyekiti huyo alisema kipimo cha ubora wa usajili watakaofanya utaonekana kupitia michuano hiyo.