Simba kutangaza itakaowatema Jumatatu

DAR ES SALAAM – KLABU ya Simba imesema kuanzia Jumatatu itatangaza wachezaji itakaoachana nao na kufuata wale ambao wamewaongezea mkataba.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally alisema wamedhamiria kuanza mapema usajili wa kikosi kuwahi maandalizi kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

“Kuanzia Jumatatu Juni 17 tutaanza rasmi kutangaza wale ambao tunaachana nao, tutafuata wale ambao wameongeza mikataba na tutamalizia na wachezaji wetu wapya ndani ya Simba,” alisema Ahmed.

Wakati Ahmed akisema hayo, dirisha la usajili kwa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa mwaka 2024/25 litafunguliwa leo na kufungwa Agosti 15, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupitia kwa Ofisa Habari wake, Clifford Ndimbo jana imesema klabu zinatakiwa kuanza kufanya usajili na uhamisho wa wachezaji wao kwa msimu wa mwaka 2024/25.

SOMA: Dirisha la usajili Bara lafunguliwa leo

“Hakutakuwa na muda wa ziada baada ya kufungwa kwa dirisha la usajili na klabu zote zinaombwa kuzingatia muda huo wa usajili na uhamisho na tunaziomba kuwasiliana na idara ya mashindano ya TFF kama kuna changamoto zozote,” ilisomeka taarifa hiyo ya TFF.

Aidha, taarifa hiyo ilisema usajili na uhamisho wa wachezaji kwa dirisha dogo ni Desemba 16, 2024 na kufungwa Januari 15, 2025.

Habari Zifananazo

Back to top button