Simba Queens yapewa ushindi mechi ya JKT
DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa miguu nchini (TFF) imeipoka alama 5 JKT Queens na kuitoza faini ya Sh 3,000,000 baada ya kugomea mchezo dhidi ya Simba Queens mnamo Januari 09, 2024.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ulipaswa kuchezwa katika Uwanja wa Chamazi complex, badala yake JKT walikaidi na kutaka mchezo upigwe katika Uwanja wao wa Major General Isamuyo ulioko Mbweni jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Kamati ya WPL chini ya TFF hii leo pia imeizawaidia Simba Queens alama 3 na mabao 3 kwa mujibu kanuni ya 18:45 toleo la 2023.
“Pia Kamati imemfungia Katibu Mkuu wa JKT Queens, Duncan Maliyabwana kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi kumi na miwili (12) kwa kuzingatia Kanuni ya 32:1.5 ya Ligi Kuu ya Wanawake Toleo la
2023,” imeeleza taarifa hiyo.
“Kamati imejiridhisha pasipo shaka kuwa Klabu ya JKT Queens ilipata taarifa za mchezo husika kuchezwa Azam Complex, Chamazi kabla ya siku ya mchezo na siku ya mchezo Januari 8, 2024 katika kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM), Mwenyekiti wa
Kikao alikumbusha juu ya muda na uwanja utakaoutumika kwa mchezo huo,” imesisitiza taarifa hiyo.
Kamati hiyo pia imejiridhisha kuwa klabu ya Alliance Girls ilifanya udanganyifu na kumtumia mchezaji Nelly Kache katika mchezo namba 3 dhidi ya Geita Queens huku ikijua fika hana uhalali wa kucheza.
“Kamati imekubaliana kuwa Alliance Girls ilifanya makosa na hivyo imepoteza mchezo huo, na Geita Queens imepewa ushindi wa alama 3 na mabao 3 kwa mujibu wa Kanuni ya 48:23 ya Ligi Kuu ya Wanawake Toleo la 2023. Pia Alliance Girls imepigwa faini ya sh. laki tano (500,000/-),” imehukumu kamati hiyo.
Kwa upande mwingine, Meneja wa timu ya Alliance Girls, Thereza Chacha ametozwa faini ya sh. laki tano (500,000/-) kwa kutoa taarifa ama nyaraka zisizo sahihi juu ya mchezaji Nelly Kache (leseni) ili kucheza katika mchezo huo. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:13 Ligi Kuu ya Wanawake kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
Mchezaji Nelly Kache ametozwa faini ya sh. laki tano (500,000/-) kwa mujibu wa Kanuni ya 42:11 kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.