Simba yaifuata CS Sfaxien kibabe

SIMBA imeondoka alfajiri leo kwenda Tunisia kupitia Uturuki kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien utakaochezwa Januari 5, mwaka huu.
Kwenye mchezo uliopita Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba ilishinda kwa mabao 2-1 na CS Sfaxien kuanzisha vurugu baada ya mechi hiyo, wakigomea bao la dakika za mwisho la Kibu Dennis.

Simba jana walifanya mazoezi asubuhi na jioni baada ya wachezaji kurejea katika mapumziko ya siku mbili.
Akizungumza na HabariLEO, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema Simba itakuwa na msafara wa watu 50 ambao 22 ni wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi.
“Tutaondoka alfajiri kesho (leo) kupitia Uturuki na Tunisia tutafika saa 10 jioni sawa na saa 12 jioni kwa saa za Tanzania,” alieleza Ally. Simba inashika nafasi ya pili kwenye kundi, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza michezo mitatu.



