Simbachawene: Msiharibu utumishi kwa maslahi binafsi
SERIKALI imekemea wakuu wa taasisi za umma wanaoharibu utumishi wa umma kwa maslahi binafsi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameagiza viongozi hao wazingatie usimamizi wa rasilimaliwatu ili kuwa na usimamizi wa rasilimali nyingine ambazo serikali imefanya uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Simbachawene ametoa maagizo hayo Dodoma wakati akifunga kikaokazi kati yake na wakuu wa taasisi za umma.
Amesema katika siku za karibuni, imejitokeza mienendo isiyo ya kawaida ikiwamo ya baadhi ya waajiri kuchagua aina ya watumishi wa kufanya nao kazi.
“Mkuu wa taasisi huna nafasi ya kumkataa mtumishi, unachotakiwa kufanya ni kumpokea na kama hawajibiki
unamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Lakini kuna kauli ya ujumla ya huyu hafai, nani kakwambia wewe unafaa?” alisema Simbachawene.
Aliongeza: “Mna haki ya kutoa mapendekezo ya sifa za mtumishi mnayemtaka ili mamlaka iamue na msilete watu kwa majina, mnaharibu. Tukichunguza tunakuta mlisoma naye kidato cha nne, mtoto wa mjomba, tukichunguza tunakuta mengi”.
Simbachawene alisema changamoto nyingine ni ya wakuu wa taasisi kukataa mtumishi aliyepangiwa kuhamia kwenye taasisi husika na kuwaombea uhamisho watumishi wenye changamoto za kiutendaji badala ya kuwachukulia hatua za kinidhamu.
“Mtumishi anakuja kuripoti kwenye taasisi zenu wewe umeshampiga mkwara afisa utumishi, mtu yeyote asiingie
hapa hadi kwa kibali changu, taasisi ni yako? Naomba sana jambo hili liachwe, linatudhalilisha, linatutia aibu,”
alisema.
Aliongeza: “Mtumishi anakuja mnaanza kusema kwani ametoka wapi, amekuja kuchunguza mambo yetu, wewe una mambo yako? Yepi? Kwenye taasisi ya umma? Katika utumishi wa umma, barua inasema siku 14 baada ya siku hizo mtumishi awe ana kiti na amepewa majukumu vinginevyo unatoa mshahara bure, wapo wengi hawapewi majukumu imepita muda mrefu hadi wengine miezi minane”.
Pia, Simbachawene alisema kuna changamoto ya wakuu wa taasisi kuondoka na rasilimaliwatu wanapohamishwa
na wanaoingia wanasema hawafai na hawawataki. Simbachawene alisema pia kuna changamoto ya kufanya kazi bila kuzingatia mipaka na mamlaka ya kisheria.
Alisema baadhi ya watendaji wakuu wa taasisi wanafanya uamuzi bila kuzingatia ushauri wa kitaalamu kutoka kwa watumishi wa chini yao pia walio juu.
“Kwenye tawala za mikoa kuna mwingiliano mkubwa sana na wakati mwingine kushindwa kujua nani anafanya nini. Kumekuwa na tatizo kubwa huko chini. Wakati mwingine DAS (Katibu Tawala wa Wilaya) naye anamfokea mkurugenzi wa halmashauri, huyu mtu ni mtu mkubwa sana,” alisema Simbachawene.
Aliongeza: “Wakati mwingine unakuta ile KUU (Kamati ya Ulinzi na Usalama) inamuita mkurugenzi na kumfokea, nyie jukumu lenu ni kumshauri tu…”



