Sirro ataka juhudi zaidi vita dhidi ya ukatili

KIGOMA; MKUU wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Kigoma kuongeza juhudi katika kushughulikia masuala ya ukatili kwa wanawake na watoto, kwani kwenye suala hilo bado mchango wa mashirika hayo ni mdogo.
Balozi Sirro amesema hayo akifungua mkutano wa mwaka wa jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo, ambapo amesema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuongeza bajeti zao katika kushughulikia vitendo vya ukatili na watoe ripoti kila wakati kwa kile walichofanya kwa jamii.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma ,Dk Rashid Chuachua, amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya ubakaji na ulawiti mkoani Kigoma na kwamba pamoja na serikali kufanya kazi kubwa kutoa elimu kwa jamii kwa kutoa taarifa na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua, lakini mashirika yasiyo ya kiserikali yana mchango mkubwa kuisaidia serikali kuhusiana na jambo hilo.
Amesema kuwa mashirika yasiyo ya serikali yanapaswa kushirikisha serikali za wilaya na mkoa, mipango na shughuli wanazofanya kushughulikia vitendo vya ukatili, ubakaji na ulawiti lakini pia watoe taarifa kwa mamlaka za serikali kuhusiana na kile walichofanya wanapotekeleza miradi yao inayohusiana na hilo, lakini shughuli nzima wanazofanya kwa jamii.
Awali akizungumza mkutano huo, Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Kigoma, Msafiri Nzunuri alisema mashirika yasiyo ya kiserikali yamefanya kazi kubwa na nzuri kuunga mkono serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali kwa jamii mkoani Kigoma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO), mkoani Kigoma, Alex Luoga alisema kuwa mashirika mengi yamekumbwa na mdororo wa fedha za kutekeleza shughuli zao, baada ya serikali ya Marekani kupunguza kwa kiwango kikubwa misaada yake kwa nchi za Afrika, hivyo mashirika ya Tanzania nayo yameathirika na hali hiyo.
Hata hivyo Luoga alisema kuwa bado mashirika yamefanya juhudi katika kutafuta fedha maeneo mengine, ili kuhakikisha yanaendelea na shughuli zao katika kuwahudumia wananchi ili kusaidia na serikali katika hilo.



