SMZ yaongeza pensheni kwa zaidi ya 100%

DODOMA – SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeongeza kiwango cha malipo ya pensheni jamii kwa kila mzee aliyefi kisha umri wa miaka 70 kwa asilimia 150 huku pensheni kwa wastaafu ikiongezeka kwa asilimia 100.
Haya yalibainishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Hemed Suleiman Abdulla wakati akielezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Novemba, 2020 hadi Desemba, 2024.
Alisema serikali imeongeza kiwango cha malipo ya Pensheni Jamii kwa kila mzee aliyetimia umri wa miaka 70 kutoka Sh 20,000 hadi Sh 50,000 ambapo utaratibu wa malipo ya Sh 50,000 yalianza mwaka wa fedha 2023/2024 sawa na asilimia 150.
Abdulla alisema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, serikali imetumia Sh bilioni 18.3 kulipa pensheni jamii kwa wazee 30,395 ambayo ni sawa na asilimia 261 ya lengo. Alisema pia pensheni ya wastaafu imeongezeka kutoka Sh 90,000 hadi Sh 180,000 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 100.



