SMZ yapunguza tozo vyakula kudhibiti mfumuko wa bei

KATIKA kukabiliana na kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa za chakula uliojitokeza nchini, Shirika la Bandari la Zanzibar (ZPC) limetangaza kupunguza kwa asilimia 80 ya tozo kwa bidhaa zote za chakula zitakazoingizwa nchini kutoka Tanzania Bara kupitia bandari zote za Unguja na Pemba.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa ZPC, Akif Khamis Ofisini kwake Malindi juzi jioni. Alisema uamuzi huo utaanza kesho hadi Novemba 24, mwaka huu.

Alisema uamuzi huo umekuja baada ya kujitokeza kwa mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu za chakula katika kipindi cha wiki moja baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Alisema agizo hilo litazihusu bandari zote zinazotoa huduma za uingizaji na usafirishaji wa bidhaa za chakula ikiwemo bandari ya Malindi, Wete na eneo la Ngalawa ambalo linasimamiwa na kampuni ya ZMT.

“Napenda kuwajulisha wafanyabiashara wote kwamba Shirika la Bandari limetangaza punguzo la asilimia 80 ya tozo ya kuingiza bidhaa za chakula katika bandari zake kwa ajili ya kutoa nafasi kuingia kwa wingi bidhaa za chakula muhimu cha binaadamu,” alisema.

Akifafanua, Khamis alisema punguzo hilo linahusu zaidi bidhaa zinazotoka Tanzania Bara na kutoka Zanzibar kuingia Bara, ikiwemo za mahitaji ya chakula cha binadamu.

Alisema tayari uongozi wa Shirika la Bandari umefanya mkutano na wawakilishi wa wafanyabiashara wa usafirishaji wa bidhaa za chakula katika Bandari ya Malindi ambao kwa ujumla wamelipokea agizo hilo na kuahidi kulitekeleza.

”Wafanyabiashara wanaojishughulisha na uingizaji wa bidhaa za chakula kutoka Bara tayari tumekutana nao na kuwajulisha agizo hilo na wao kwa ujumla wamelipokea kwa mikono miwili,” alisema.

Kutokana na vurugu zilizojitokeza Tanzania Bara katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, uingiaji wa bidhaa muhimu za chakula kutoka Tanzania Bara ulisita na kusababisha mfumuko mkubwa wa bei ya bidhaa, kiasi cha wananchi kulalamika na kuitaka serikali kuingilia kati.

Bidhaa ambazo bei yake iliongezeka mara dufu na wakati mwingine kukosekana moja kwa moja ni viazi ambavyo ni chakula maarufu kwa wakazi wa Zanzibar na nyanya ambazo zote kwa asilimia 90 zinaingizwa nchini kutoka Tanzania Bara.

Wakala wa usafiri wa majahazi, Ali Haji alisema wameanza kupokea bidhaa za vyakula kutoka Tanzania Bara katika kipindi cha siku tatu sasa kwa ajili ya mahitaji ya ndani.

“Nimepokea zaidi ya majahazi 10 yakiwa na shehena ya bidhaa za chakula na nafaka ikiwemo viazi, nyanja na unga wa sembe ambapo katika kipindi cha wiki mbili zijazo hali ya upatikanaji wa bidhaa utakaa sawa na kuondokana na mfumuko wa bei uliojitokeza,” alisema Haji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button