Spika ‘apiga pini’ kuteta na Waziri Mkuu bungeni

DODOMA; SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amezuia wabunge na mawaziri kwenda kuzungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, wakati wa kipindi cha maswali na majibu kikiendelea.

Pia Spika Tulia ametoa maelekezo wabunge wanaotaka kuzungumza na Waziri Mkuu akiwa ndani ya ukumbi wa bunge, hawatakiwi kutumia zaidi ya dakika mbili na kinyume cha hapo atawataja kwa majina.

Spika Tulia ametoa maelekezo hayo bungeni leo Mei 30,2024, alipokuwa akijibu muongozo wa Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda.
Mbunge huyo amesema mara kwa mara Spika amekuwa akiwaelekeza wabunge kuacha kutumia muda mrefu kuzungumza na Waziri Mkuu, hali ambayo wakati mwingine inavuruga mijadala, hivyo kuomba muongozo baada ya maonyo na maelekezo mbalimbali ya Spika jambo hilo bado linaendelea, nini kitafuata.

Akijibu muongozo huo, Spika Tulia amesema ni kweli ameonya mara nyingi suala la wabunge na mawaziri kwenda kuzungumza na Waziri Mkuu wakati wa kipindi cha maswali na majibu na kusema jambo hilo wakati mwingine linafanya baadhi ya mawaziri kushindwa kufuatilia maswali ya nyongeza yanayoelekezwa maeneo yao.
Pia amesema baadhi ya wabunge wamekuwa wakitumia muda mwingi kuzungumza na Waziri Mkuu, huku pia wakati Waziri Mkuu akitoka nje ya ukumbi kwa dharura, baadhi ya wabunge wanasimama, hali inayofanya Waziri Mkuu apite kwa kila mmoja kumsalimia na hivyo kuingilia mijadala.

Kutokana na hali hiyo Spika Tulia, ametaka wabunge na mawaziri wakati wa kipindi cha maswali na majibu wasiende kwenye meza ya Waziri Mkuu, lakini pia wakati wa mijadala mingine wakienda wahakikishe hawatumii zaidi ya dakika mbili.

Pia amesema ikitokea Waziri Mkuu anaondoka kwa dharura wakati bunge likiendelea wasisimame, maana wakifanya hivyo atalazimika kumsalimia kila mmoja, hivyo kuchelewesha dharura yake na kutania kuwa pengine amepigiwa simu na Rais, ni vyema kama kuna mtu ana ulazima akaenda naye nje kusikiliza simu.

Habari Zifananazo

Back to top button