Sugu awarejesha Daz Nundaz jukwaa moja

DAR ES SALAAM – RAPA mkongwe nchini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amewakutanisha wasanii wa kundi la Daz Nundaz na sasa wanatarajia kuimba pamoja usiku wa wakongwe Julai 19 mwaka huu, Warehouse, Masaki, Dar es Salaam.

Kundi hilo linaundwa na Feruzi Mrisho ‘Feruzi’ na David Nyika ‘Daz Baba’ ambapo lilifanya vizuri miaka ya 2000 kabla ya baadaye kusambaratika na kila mtu kuimba kivyake.

Sugu alisema wasanii hao wanapaswa kuheshimiwa kwa kuandaliwa tamasha linaloitwa ‘Bongo Fleva Honors’ kwani ni miongoni mwa wasanii waliochangia kukua kwa muziki wa bongo fleva nchini.

Advertisement

“Hawa ni wakongwe wasio na shaka kutokana na mchango wao katika muziki wa bongo fleva tangu kuanza kwake, kukua na kukomaa, bado wapo na wanaendelea kushindana na wengine sokoni,”alisema.

Nyimbo zao maarufu zilizowahi kutamba miaka ya nyuma ni Starehe, Barua, Maji ya shingo, Namba nane, Nipe tano na Elimu dunia.

Sugu amehimiza mashabiki wa muziki kujitokeza siku hiyo kwa wingi kuwapa heshima wasanii hao kwani wataimba ‘live’ nyimbo zao zote zilizofanya vizuri huko nyuma.