DAR ES SALAAM; SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limeingia mkataba wa makubaliano na taasisi za elimu za umma na mashirika yasiyo ya kiserikali 11 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya.
Akizungumza wakati wa utiaji saini mikataba hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mwakilishi Mkaazi wa WHO nchini, Dk Charles Sagoe amesema malengo ya makubaliano hayo ni kuimarisha mifumo ya afya, ili kuongeza uwezo na ufanisi wa mifumo ya afya.
“Hii ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya,kuimarisha maendeleo ya wafanyakazi wa afya, na kukuza matumizi ya teknolojia ya ubunifu katika utoaji wa huduma za afya,” amesema.
Amesema eneo lingine ni kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, ikiwa ni pamoja na juhudi za ushirikiano katika maeneo kama vile chanjo, ufuatiliaji wa magonjwa, mwitikio wa mlipuko, na kukuza afya ya mitindo ya maisha.
“Kingine ni ukuzaji wa afya na elimu tutaunganisha nguvu kuinua uhamasishaji na kukuza elimu ya afya miongoni mwa Watanzania. Hii ni pamoja na mipango ya kushughulikia viashiria muhimu vya afya,kama vile lishe, usafi wa mazingira, usafi na afya ya uzazi,” amesema.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ambele Mwakilango amesema tukio hilo litaondoa matatizo katika sekta ya afya na Wizara ya Afya ni sehemu ya kuunganisha wadau wanapofanya kazi nchini.
“Tunaangalia kama kazi zao zinakidhi vigezo na wizara itaangalia ni wapi wanatakiwa kufanya, ili kuwe na usawa wa utoaji huduma, WHO wametusaidia kupata hawa watu, mwaka 2025 tuna vipaumbele vya wizara na wadau watafanyia kazi,” amesema.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni kupata watumishi wa afya, bima ya afya kwa wote ,huduma bora za afya hivyo wataendana na vipaumbele vya wizara.
Taasisi zilizoingia Mkataba huo ni Ndaki ya Elimu Chuo cha Dar es Salaam(DUCE), Catholic Relief Services(CRS) Doctors with Afrca-CUAMM SIKIKA na Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Nyingine ni Tanzania Health Summit, AMREF Africa in Tanzania, International Rescue Committee, Ifakara Health Institute(IHI, Raising up Friendship Foundation (RUFFO) na Chuo Kikuu cha Sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS).